Skip to main content
News and Events

DKT TIZEBA AZUIA HALMASHAURI KUTOA VIBALI VYA UNUNUZI WA KAHAWA

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) amezuia Halmashauri zote nchini kujihusisha na utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara vya kununua kahawa kwa wakulima.

 

Dkt Tizeba ametoa zuio hilo Leo tarehe 7 Octoba 2018 wakati akihutubia maelfu ya wanachi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uwanja wa Changarawe Wilayani Karagwe wakati wa muendelezo wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) aliyoianza Jana tarehe 6 Octoba 2018 mkoani Kagera.

 

"Wafanyabiashara wa kahawa ili wanunue zao hilo walikuwa wanaenda kuomba kibali cha ununuzi kilichokuwa kinatolewa na Halmashauri za wilaya, Hili jambo tumelitafakari na wenzangu wa Wizara hususani watendaji pamoja na Bodi ya kahawa tumeona halina maana tena" Alikaririwa Dkt Tizeba

 

Waziri Tizeba alisema kuwa Wafanyabiashara hawana sababu ya kuomba vibali kwenye Halmashauri vya kununua kahawa badala yake itatosha kuwa na leseni ya biashara ya Kahawa inayotolewa na Bodi ya Kahawa Tanzania, jambo ambalo linawatambulisha wafanyabiashara kwamba wanalipa kodi.

 

"Sasa hivi tunaingia kwenye mfumo wa ushirika hivyo Wafanyabiashara watanunua kahawa kupitia mfumo huo mahususi hivyo hakuna sababu ya kusumbuliwa na Halmashauri kwa kupewa vibali" Alisisitiza

 

Aidha, Kuhusu kahawa ya madaraja ya chini, Waziri Tizeba alisema kuwa kahawa hiyo kwa kipindi kirefu imekuwa ikizuiliwa kuuzwa nje ya nchi. Hivyo kwa mujibu wa utafiti wa kubaini namna inavyotumika nchini ilibainika kuwa kahawa hiyo inanunuliwa na watu wachache ambao ndio wanaratibu utaratibu wa kuuza nje huku waliokoboa wakizuiwa kuuza nje.

 

"Jambo hili sio sawa, sisi tunachotaka wakulima washiriki kwenye mnyororo wa thamani utakaowafanya wawe na uwezo wa kutafuta mnunuzi nchini au nje ya nchi watakapopewa bei nzuri" Alisema

 

Dkt Tizeba aliongeza kuwa Kahawa hiyo itauzwa popote Duniani kutegemea na kiasi cha fedha kitakachokuwa rafiki na chenye tija kwa mkulima.