Skip to main content
News and Events

Dkt. Mary Mwanjelwa - Tumieni Ushirika kupiga vita adui njaa, ujinga, maradhi na umaskini

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa amewataka Washiriki wa Mkutano wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), kuvitumia Vyama hivyo kama silaha ya kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo ya kweli.

Dkt. Mary Mwanjelwa ambaye ndiye mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kuadhimisha Uanzishwaji wa Vyama vya Akiba na Mikopo amesema hakuna ubishi kuwa mafanikio yaliyopatikana kupitia Vyama hivyo yanadhihirisha kuwa ni njia madhubuti ya Wananchi katika kupambana na adui njaa, ujinga, maradhi na umaskini.

Dkt. Mwanjelwa amekaririwa akisema “Nimetembelea mabanda kadhaa ya Vyama vya Akiba na Mikopo kutoka Taasisi za Umma kama Ngome SACCOS, TANESCO SACCOS, Bandali SACCOS, wameniambia kiasi cha mitaji waliyonayo ni unazungumzia mabilioni ya Shilingi za Kizanzania, ambapo Wanachama wanakopeshana kwa riba nafuu na kwa muda mzuri”

“Jambo hilo linatia moyo na niwaombe Viongozi na ninyi Wanachama ambao mmejiunga kwenye Vyama vya Akiba na Mikopo kuwahamasisha wengine kujiunga na Vyama vya Akiba na Mikopo ili tuongeze wigo wa idadi kubwa ya Watanzania”. Amekaririwa Naibu Waziri.

“Na kama Watanzania wengi watajiunga basi tutakuwa na nafasi kubwa kama Taifa kupambana na maadui hawa watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini”. Amekaririwa Naibu Waziri Dkt. Mwanjelwa.

Aidha, Naibu Waziri, Dkt. Mwanjelwa ameuagiza Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini Bwana Tito Haule, kuhakikisha anaitumia nafasi ya kuelimisha umma kuhusu faida na uzuri wa USHIRIKA kupitia Vyama vya Kuweka na Kukopa kama ndiyo silaha ya kupeleka mbele maendeleo ya Ushirika nchi.

“Mrajis elimu kwa Umma ni jambo la muhim sana, hata kama mnafanya mambo mazuri lakini kama Wananchi hawatafahamu kuhusu faida na mambo mazuri yanayohusu kujiunga na Vyama vya Akiba na Mikopo itakuwa ni kazi bure, fanyeni kila linalowezekana ili kuwaelimisha Watanzania”.

Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa USHIRIKA pia ni njia ya kuongeza tija na uzalishaji katika mazao ya kilimo na kwa njia hiyo, uzalisahaji wa mazao ya kilimo kwa ajili ya viwanda vya kati na vikubwa unaweza kuongezeka kwa kutumia Vyama vya Akiba na Mikopo.

“Msisahau kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamilia katika kulifikisha Taifa kwenye uchumi wa viwanda na Watanzania wengi wanaojihusisha na Sekta ya Kilimo ni zaidi ya asilimia 75 kwa maana hiyo, Vyama vya Akiba na Mikopo pia vitumike katika kuongeza tija na uzalishaji wa malighafi za viwanda vya usindikaji vidogo, vya kati na vikubwa”. Amemalizia Dkt. Mary Mwanjelwa.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) yalianza rasmi jana tarehe 18 Oktoba na yanafikia kilele leo tarehe 19 Oktoba, 2017 katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, Mjini Dodoma.