Skip to main content
News and Events

Kilimo Kuwashirikisha Farm Africa kwenye ASDP II

Wizara ya Kilimo imekutana na Shirika linaloshughulikia kilimo la Farm Africa lengo likiwa ni kuona namna bora ya kushirikiana katika kuendeleza sekta ya kilimo hapa nchini.

Akiongea kwenye mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Kilimo I hivi karibuni, Mkurugenzi wa  Sera na Mipango Bi Janeth Simkanga amesema Shirika hilo limekuwa likifanya shughuli nyingi za kilimo  ikiwemo kupeleka teknolojia, kutafuta masoko ya wakulima na kuongeza thamani ya mazao katika mikoa mbalimbali ikiwemo Manyara, Tabora na Arusha lakini hapakuwa na ushirikiano na Wizara ya Kilimo.

Alisema  imefika wakati wa Wizara ya Kilimo kuwatambua wadau wake na kujua wanachokizalisha  ili waweze kuingia katika mfumo wa program yakitaifa ya  kuendeleza kilimo hapa nchini (ASDP II)

Mkurugenzi wa kampuni hiyo hapa nchini Bwana Stive Ball wakati wa wasilisho lake amesema shirika hilo linashughulika na uendelezaji wa kilimo na maliasili, uongezaji wa thamani ya mazao, matumizi ya Tehema (ICT) katika kuendeleza kilimo, uhifadhi wa mazingira  (CSA) na utafutaji wa masoko ya wakulima.

Aidha shirika hili limekuwa lishughulikia mazao ya mahindi, mpunga, ufuta, maharage na Uyoga  na wamekuwa wakishirikiana na vituo mbalimbali vya Utafiti wa Kilimo pamoja na Wakala wa Mbegu wa Taifa (ASA) ili kupata mbegu bora alisema bwana Stive.

Naye Tumaini Elibariki Meneja wa Programu wa Shirika hilo amesema wakulima wengi wamepata mafunzo juu ya matumizi ya simu za kisasa (smart phone) ambazo zimewekewa programu maalum yenye kufundisha namna mbalimbali kuhudumia mazao.

Aidha kufuatia teknolojia hiyo  wakulima wameweza kufundishana kupitia simu hizo na  tija kubwa imepatikana alisisitiza Bwana Tumaini.