Skip to main content
News and Events

MKOA WA PWANI NA MKAKATI WA KUKUZA ZAO LA MUHOGO

Mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa ya Tanzania bara inayoongozwa kwa uzalishaji mkubwa wa zao la Muhogo. Mikoa mingine ni Tanga, Lindi, Mtwara, Morogoro na mikoa ya Kanda ya Ziwa. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa sasa inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuongeza tija na uzalishaji ikiwemo kuongeza uzalishaji kutoka tani sita kwa hekta moja hadi kufikia tani kumi na tano mpaka ishirini. Aidha, serikali inashauri wakulima wote wa zao la muhogo na mazao mengine kuzalisha mazao yao kwa kuangalia mahitaji ya soko ikiwa ni pamoja na kuzalisha mazao ya kutosha, udhibiti wa visumbufu vya wadudu, magonjwa pamoja na usafi wa mazao hayo. Pia serikali kwa kushirikiana na wadau wengine imekuwa ikiainisha masoko ya ndani na nje ili mkulima aweze kuboresha kilimo chake na kulifanya soko liwe la uhakika. Hivi karibuni soko la muhogo limeongezeka kwa mfano Tanzania imepata fursa ya kuuza muhogo nchini China, masoko hayo yanahitaji kiwango kikubwa cha muhogo lakini wenye sifa stahiki. Ni kwa muktadha huo mkoa wa Pwani umeanza uhamasishaji wa uwekezaji katika zao la muhogo ili kuwawezesha wakulima kujiongezea kipato na wakati huo kuendanana soko la China. Hali hiyo imebainika hivi karibuni wakati maofisa kutoka Wizara ya Kilimo walipotembelea mkoa huo ikiwa ni mkakati wa wizara kuhamasisha ulimaji zao la muhogo na kuangalia changamoto zake kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo. Akielezea harakati za wilaya ya Kibiti katika kuhamasisha zao la muhogo, Afisa Kilimo wa Wilaya Bwenda Ismail alisema uhamasishaji huo unaenda sambamba na utoaji mafunzo, utoaji mbegu bora kwa wakulima pamoja na kuhakikisha kila kaya inakuwa na hekari moja ya muhogo jambo litakalongeza uzalishaji. Kwa mujibu wa Ismail, sasa hivi zao la muhogo katika wilaya ya kibiti limekuwa la kibiashara na hali hiyo inatokana na usafirishwaji wa muhogo mbichi kwa wingi kila siku kutoka wilaya hiyo kuenda Dar es Salaam. Hatua nyingine inayofanywa na halmashauri ya wilaya ya Kibiti ni kusaidia wakulima katika uuzaji muhogo hasa baada ya kubainika wakulima wilayani humo wanapunjwa wakati wakuuza muhogo kwa wafanyabiashara. Wilaya imejenga soko la pamoja lililogharimu milioni 65 na mategemeo ni kuwa muhogo utauzwa kwa vipimo stahiki tofauti na sasa ambapo wakulima wanapunjwa kwa mihogo kutenganishwa ile mikubwa na midogo. Afisa kilimo huyo wa wilaya ya Kibiti alisema, uhamasishaji umewekwa pia katika ujenzi wa viwanda lengo likiwa kuhakikisha muhogo unaonunuliwa kutoka kwa wakulima unasindikwa sambambana kuhakikisha wilaya ya kibiti m inatenga maeneo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi, wawekezaji wakubwa, wakati na wadogo pamoja na maeneo kwa ajili ya vijana na msisitizo ukiwa kila kata kutenga eneo. Alibainisha kwa kueleza kuwa, wilaya ya Kibiti pia inaimarisha vikundi vidogo vidogo kwa kuitumia asilimia kumi ya mfuko wa vijana na wanawake kuwapatia mikopo ambapo asilimia tano inaenda kwa wanawake na inayobaki kwa vijana na kuweka wazi kuwa kutokana na zao la muhogo kuleta tija kwa sasa wilaya ina vikundi vya usindikaji vitano na kuvitaja kuwa Mivinjeni, Sururu farmers, Dimani, Lugungu na Kigunguli ambavyo viko katika uboreshaji Pia halmashauri inatoa elimu ya ujasiriamali ili wakulima kuondokana na zana iliyojengeka awali kuwa muhogo ni zao la kinga ya njaa na kutengeneza mipango kuwaunganisha wakulima na taasisi za kibenki ili kupata mikopo yakuendeleza shughuli zao, pia kuwahamasishawakulima kukopa zana za kilimo kutoka mfuko wa pembejeo wa taifa ambapo wakulima wanaweza kukopa trekta badala ya kutumia jembe la mkono utakaosadia kuongeza eneo, Kwa sasa Wilaya ya Kibiti umekamilisha sheria ndogo ambapo kila kaya itatakiwa kulima zao la muhogo jambo litakalosaidia kusukuma watu kuingia shambani ikiwemo vijana ambapo sasa watalazimika kuingia katika kilimo na kuacha kukaa katika ‘’gogo zembe’’ ili kuendana na kasi ya Tanzania ya viwanda na soko la china la muhogo kwa kuzalisha muhogo wa kutosha. Ili kuvutia uwekezaji na kukabiliana na changamoto ya umeme, Afisa Kilimo wilaya ya Kibiti alisema, wakati serikali inafanya juhudi za kurekebisha mitambo ya songas wao kama wilaya wameomba kuunganishwa na gridi ya taifa ili kuwa umeme wa uhakika utakaowezesha wawekezaji kuja kuwekeza sambamba na kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki kwa kurekebishwa barabara zinazoenda vijijini. Kwa upande wa wilaya ya Mkuranga, serikali wilayani humo katika bajeti yake imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kununua na kusambaza mbegu za muhogo kwa wakulima mbalimbali. Kwa mujibu wa Afisa Kilimo wilayani humo Bi. Julita Bulali kufuatia jitihada za wilaya yake kusambaza mbegu kwa wakulima kumekuwa na mwitikio mkubwa wa watu kuwekeza katika zao la muhogo. Hata hivyo, changamoto kubwa katika wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani ni kusitishwa kwa uzalishaji/usindikaji muhogo katika kiwanda cha Ukaya farm ambacho imekuwa mkombozi mkubwa wa kununua muhogo kutoka kwa wakulima kutokana na kukosekana kwa umeme katika kiwanda hicho. Kwa mujibu wa meneja wa kiwanda hicho Joseph Mtanga, awali kiwanda hicho kilikuwa kikitumia jenereta lakini mara baada ya kuharibika najitihada za kupata umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kushindikana shughuli za kiwanda zimesimama na hivyo kuwakosesha wakulima kuuza muhogo katika kiwanda hicho. Meneja huyo wa kiwanda cha Ukaya Farm alisema kiwanda chake hununua wastani wa tani nne mpaka mpaka kumi na mbili kwa siku za muhogo kutoka kwa wakulima na kusitishwa kwa usindikaji kumesababisha pia ajira za watu thelathini mpaka arobaini kusimama. Baadhi ya wakulima mkoani humo walisema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa soko la uhakika na mfumo mbaya mbaya wa ununuzi wa mazao yakiwa bado shambani jambo linalosababishwa mzunguko wa biashara kutoenda vizuri. Mkulima wa mbegu za muhogo aina ya Kiroba kutoka eneo la Nyanduturu Sultan Chuga ameeleza kuwa kilimo cha muhogo wilayani humo kina faida lakini kusitishwa kwa uzalishaji katika kiwanda cha Ukaya Farm uliosababishwa na kukosekana kwa umeme kumekuwa tatizo kubwa kwake na wakulima wengine. Alisema yeye amelima hekari tatu za mbegu ya muhogo lakini amefanikiwa kuuza nusu heka na kubainisha kuwa anashindwa kuuza mihogo yake kwa sababu soko lake lipo kwenye usindikaji pekee na siyo kwa wafanyabiashara wa chakula ambao hawapendei biashara hiyo. Aidha, Juma Mteta kutoka kikundi cha Mivinjeni kilichopo kata ya Bungu wilaya ya Kibiti alisema, biashara ya muhogo wakati mwingine inakwama kutokana na masuala ya kisera ambapo bidhaa zao zinahitaji kuidhinishwa na shirika la viwanga Tanzania (TBS) jambo linalofanya kushindwa kuingia katika ushindani kutokana na kutokidhi vigezo. Pia ukosekanaji wa vipimo stahiki katika uuzaji muhogo katika magari unawanyonya wakulima kwa kuwa bei wanayakubaliana mazao yakiwa shambani tofauti na bei wanayouza. ‘’katika soko hakuna vipimo stahiki wakati wa uuzaji katika magari na matenga, vipimo siyo rafiki kuna steka unaambiwa gari milioni moja kumbe unatamanishwa tu baadaye unaambiwa mihogo yako ina mizizi na hawaiachi’’ alisema Mteta. Kwa miaka mingi zao la muhogo limekuwa likitumika kama zao la kinga ya njaa ambapo wakulima walikuwa wakilima zao hilo kwa sababu ya upungufu wa mvua. Kipindi hicho kipaumbele kiliwekwa katika zao hilo hasa baada ya mazao kama mpunga na mahindi kuwa kwenye wakati mgumu kwa kushindwa kustawi kwa sababu mbalimbali ikiwemo magonjwa na sababu nyingine. Na kipindi chote zao la muhogo limekuwa likitumika kama zao la chakula cha njaa lakini sasa hali imebadilika. Watafiti kutoka wizara ya kilimo wamekuwa wakibuni matumizi mengi ya zao la muhogo pamoja na aina nyingi za muhogo zenye ladha nzuri, uwezo wa kuvumilia ukame na hata ambazo ni kinzani na magonjwa kama batobato na michirizi ya kahawia. MWISHO