Skip to main content
News and Events

Tafuteni Majawabu Ya Kero Za Wananchi - Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Awaagiza Watumishi!

- Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba (Kushoto) wakati anawasili Wizarani. Katikati ni Katibu Mkuu, Bibi Sophia Kaduma, na Kulia ni Katibu Mkuu Dk. Yohana Budeba
- Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba (katikati), akisisitiza jambo wakati akizungumza na Wakuu wa Idara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi (hawapo pichani)
- Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba (wa tisa kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba amewataka wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi, kutumia muda wao kuhangaikia kutafuta majawabu ya matatizo ya wananchi.  Aliyasema hayo wakati anaongea na Wakuu wa Idara za kilimo, mifugo na Uvuvi mara baada ya kuwasili Wizarani hapo kufuatia alipoteuliwa kuiongoza Wizara hiyo. 

Katika hotuba yake aliyoitoa baada ya kukabiribishwa na Wafanyakazi wa Wizara hiyo, Mheshimiwa Waziri alionya kuwa hizi siyo zama za kufanya kazi kwa mazoea ambapo kila mtumishi anatakiwa kusugua kichwa kutafuta majawabu ya kero za wakulima, wafugaji na wavuvi ambao ni zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania. 

Alisema, ipo dhana iliyojengeka miongoni mwa watumishi wa Serikali kuwa muda mwingi wanahangaika kutafuta “majibu” badala ya “majawabu” ya matatizo yanayo wakabili wananchi. Akitoa mfano wa maelezo yake alisema, pembejeo za kilimo zinapochelewa kufika kwa wakulima jibu linaweza kutolewa kuwa makampuni na wakala wa pembejeo hawakupeleka mbolea kwa wakati. Hilo linaweza kuwa ni jibu lakini siyo jawabu au suluhisho la tatizo kwa wakulima ambao wameshindwa kutumia mbolea kuendena na msimu wa kilimo. 

Katika hotuba yake, aliwataka watumishi katika kila eneo kupitia kero zinazowakabili wananchi na kuweka mikakati ya kuzishughulikia kero hizo katika muda mfupi. 

“Nataka katika kipindi cha siku saba muainishe kero na mikakati yake ya kuzitatua ili tupate matokeo kwa haraka” alisema Mheshimiwa Nchemba. 

Katika moja ya mambo yanayotakiwa kushughulikiwa kwa haraka ni pamoja na kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo inazidi kukua kila siku kwa kuzingatia kuwa ardhi haiongezeki, hali ya hewa inabadilika, wakati watu na mifugo inaongezeka.  Hivyo, lazima hili tatizo lipatiwe suluhisho kwa haraka na kama kuna kitu  kinakwamisha lazima kielezwe ili kiondolewe,  alisema Mheshimiwa Nchemba.   

Mheshimiwa Nchemba alihitimisha, kwa kuwataka watumishi kujituma na kufanyakazi kwa ushirikiano wa hali ya juu ili kupata mafanikio yanayohitajika. 

Naye, Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Tate Olenasha alisema, falsafa ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano, ni kufanya jambo kwa haraka, kwa wakati na kupata matokeo sahihi na tija kwa kuzingatia maslahi mapana kwa umma. 

Alisema, mathalani unapolima shamba, kazi inakuwa imefanyika, lakini kinachotegemewa ni kupata mavuno ambayo mwisho wa siku yatatumika kuwapatia chakula Watanzania.  Aliwataka wafanyakazi wa Wizara hiyo kuzingatia falsafa hiyo wanapotekeleza majukumu yao ili mwisho wa siku wananchi waone mabadiliko katika maisha yao.

Mara baada ya kuwasili Wizarani hapo, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri walipokea maelezo ya shughuli za kilimo yaliyotolewa na Katibu Mkuu Bibi Sophia Kaduma, ambapo maelezo ya shughuli za Mifugo na Uvuvi yalitolewa na Katibu Mkuu Dk. Yohana Budeba.