Skip to main content
News and Events

Zana za Kisasa Kuwainua Wakulima

Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika chini ya Idara ya Zana za Kilimo imeandaa mkakati wa kuboresha sekta ya kilimo ili wakulima waondokane na jembe la mkono na kutumia zana za kisasa ikiwa ni moja ya sababu zinazoweza kuleta tija kwenye sekta ya kilimo nchini.

Zana ambazo zimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa na kutumia mafuta ya dizeli zinaweza kutumika katika mazingira mbalimbali ya kilimo nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya zana za kilimo ya Savoy Farm Ltd Bw. Omari  Issa akizungumza katika maonesho ya Nane Nane , viwanja vya Nzuguni alisema mashine aina ya ‘palleting’ zimetengenezwa kwa ajili ya kuwakomboa wajasiriamali wadogo wanaojishughulisha na kilimo ili wazitumie katika shughuli zao.

Alisema mashine hizo zinatumia muda mfupi katika kukoboa  mpunga na hivyo kurahisisha shughuli za mkulima.

‘’Tumetengeneza mashine za gharama nafuu ambazo zinawasaidia wakulima wa mpunga kukoboa nafaka kwa muda mfupi, hivyo aliwasihi wakulima  kuzitumia ili warahisishe shughuli zao za kilimo’’, alifafanua Bw. Omary.

Alifahamisha  kuwa mashine hizo zitasaidia kuongeza uzalishaji wa chakula katika maeneo mbalimbali nchini,na lengo la kutengeneza mashine hizo ni kuwawezesha  wakulima kuondoka kwenye matumizi ya  teknolojia ya zamani ya ukoboaji  kwa kutumia mikono na kujiunga kwenye teknolojia ya kisasa.

Kwa mujibu wa Bw. Omary mashine hizo zinatakiwa kwa wingi na  amewaomba wakulima kununua  zana bora za kilimo zinazotengenezwa nchini ili kupunguza gharama za kuagiza nje ya nchi.

Mmoja wa wakulima kutoka wilaya ya Manyoni  aliyehudhuria maonesho hayo  ,Bi. Salome Kazimoto alisema mashine za kukobolea mpunga zinasaidia kupunguza muda wa kukoboa kwa kutumia teknolojia ya zamani ambayo inachangia kurudisha nyuma  ufanisi wa kazi.

Bi. Kazimoto alikiri kuwa mashine hizo zinamrahisishia  kazi mkulima na kusema kuwa mpaka sasa idadi ya wakulima wanaotumia zana za kisasa ni wachache ikilinganishwa na idadi ya wanaotumia zana za zamani za kilimo.

Baadhi ya wakulima wanaoshiriki kwenye maonesho haya  ya kilimo wameitaka serikali kuelimisha wananchi ili watumie zana za kisasa katika shughuli zao.

‘’Endapo wakulima wataelimishwa ili watumie zana za kisasa za kilimo ili kujikwamua katika kilimo cha zamani kwa lengo la kuongeza uzalishaji’’aliongeza Bi. Kazimoto ambae ni mkulima.

Noel John, mkulima  kutoka  Morogoro alisema tangu  aanze kutumia mashine za kisasa katika shughuli mbalimbali za  kilimo katika zao la mpunga,amekuwa akifanya kazi hizo kwa muda mfupi na kwa ufanisi mkubwa.