DKT TIZEBA AKEMEA UDANGANYIFU KWENYE TASNIA YA MBEGU

Waziri wa kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) amekemea udanganyifu unaofanywa kwenye tasnia ya mbegu zinazotolewa na serikali kwa wananchi kwa bei nafuu huku wafanyabiashara wakijiingiza katika biashara ya mbegu hizo za serikali na kupandisha bei kinyume na utaratibu.

Waziri Tizeba ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kamati ya Menejimenti ya Taasisi ya kudhibiti Ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI) katika ukumbi wa AVRDC Mjini Arusha.

Aliwataka wajumbe wote wa kamati ya Menejimenti ya TOSCI kusimamia wajibu wao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha gharama za mbegu zinaendelea kupungua zaidi ili kurahisisha upatikanaji mbegu hizo kwa wananchi.

Alisema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kuwainua wakulima nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa Zana za kilimo sambamba na mbegu za Mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

"Wapo wafanyabiashara wanalima mahindi baadae wanapaka rangi Mazao hayo halafu wanayaingiza mtaani kufanya biashara kama mbegu jambo hili ni kinyume na utaratibu hivyo watendaji wote wanapaswa kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kuwakamata wadanganyifu wa namna hiyo, lakini nasisitiza tena wajibu wenu ni kuhakikisha kunakuwa na unafuu wa gharama za mbegu" Alikaririwa Mhe Tizeba na kuongeza kuwa

"Ni lazima kuwe na urahisi wa upatikanaji wa mbegu kwa wananchi ili kutekeleza matakwa ya uelekeo wa uchumi wa kati kufikia mwaka 2022"

Pia, amekemea kuhusu urasimu katika uthibitishaji wa mbegu kwa wazalishaji au waliopo katika utafiti, lakini pia wanaoomba kuingiza mbegu ndani ya nchi kutokana na uchache wa mbegu au kutopatikana kwa mbegu zinazoingizwa, kwa mantiki hiyo amekemea kikwazo cha urasimu katika uzalishaji wa mbegu.

Serikali imeendelea kusogeza huduma za upatikanaji wa mbegu kwa wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kutii Sheria bila shuruti.

Dkt Tizeba aliongeza kuwa kutokana na umuhimu wa TOSCI kwa ustawi wa kilimo ni vyema chombo hicho kikasimamiwa vyema ili dhamira ya kuwahudumiwa wananchi na kurahisisha upatikanaji wa mbegu unatekelezwa kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2015-2020 inayoielekeza serikali kuimarisha sekta ya kilimo.

Katika hafla hiyo pia Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba alizindua Nembo na wavuti maalumu ya Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa mbegu Tanzania (TOSCI).