RASIMU YA SALAAM ZA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA MHESHIMIWA CHARLES
KEENJA WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO WA TATU WA SEKTA YA PAMBA JIJINI MWANZA
TAREHE
2 MEI 2002
Mheshimiwa
Fredrick T. Sumaye (Mb.),
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa
Balozi George Kahama (Mb.), Waziri wa
Ushirika
na Masoko,
Mheshimiwa
Stephen J. Mashishanga, Mkuu wa Mkoa
wa
Mwanza,
Mheshimiwa Raphael N. Mlolwa (Mb.) Mwenyekiti wa Bodi ya
Pamba,
Mheshimiwa
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza,
Waheshimiwa
Mawaziri,
Waheshimiwa
Makatibu Wakuu,
Waheshimiwa
Wabunge,
Waheshimiwa
Wakuu wa Mikoa,
Waheshimiwa
Wakuu wa Wilaya,
Waheshimiwa
Viongozi wa Serikali,
Waheshimiwa
Wageni waalikwa,
Mabibi na
Mabwana.
1. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa niaba ya Wizara ya Kilimo na Chakula, kwa niaba yangu
binafsi na kwa niaba ya wajumbe wote wa mkutano huu nina furaha sana
kukukaribisha kwenye Mkutano huu wa Tatu wa Sekta ya Pamba. Aidha, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kutenga muda katika
shughuli zako nyingi kuja Mwanza kushiriki na kuongoza mkutano huu wa tatu wa
Wadau wa Pamba. Asante sana na karibu
sana Mwanza na kwenye Mkutano huu.
2. Mheshimiwa Waziri Mkuu, tulipokutana hapa mwaka jana, uzalishaji wa pamba nchini
ulikuwa umeshuka kutoka marobota 532,000 yaliyopatikana katika msimu wa 1992/93
hadi kufikia marobota 196,000 katika msimu wa 1999/00. Katika msimu wa 2000/01 uzalishaji ulipanda
kidogo kufikia marobota 225,000. Kwa
msimu wa ununuzi wa 2001/02, ambao ndio unamalizika, uzalishaji wa pamba nchini
uliongezeka tena hadi kufikia marobota 282,000, ongezeko la silimia 25. Hata hivyo, ongezeko hili ni chini ya
matarajio yetu ambayo yalikuwa kuzalisha marobota kati ya 400,000 na 500,000.
3. Mheshimiwa Waziri Mkuu, matarajio yetu hayakuweza kufikiwa kwa sababu ambazo
zimetajwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba hususan uhaba mkubwa wa madawa ya
kuulia wadudu katika msimu uliopita, suala ambalo lilipelekea asilimia kubwa ya
pamba kutonyunyiziwa madawa ya kuulia wadudu kabisa na hivyo kuathirika sana
kutokana na uharibifu wa wadudu wa pamba.
4. Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na
mambo mengine, madhumuni makubwa ya mkutano huu ni kutathmini maendeleo ya
sekta ya pamba ya kufuatilia utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa kwenye
Mkutano wa Pili wa Sekta ya Pamba uliofanyika mwaka jana. Mkutano huu
utazingatia zaidi juhudi zinazochukuliwa katika kuikwamua Sekta ya Pamba
kutokana na matatizo makuu matatu yaliyoainishwa na Mheshimiwa Rais katika
hotuba yake kwa mkutano huu mwaka juzi ambayo ni:- kushuka kwa uzalishaji, tija
na ubora wa pamba; usimamizi hafifu wa sekta ya pamba katika hatua zote za
uzalishaji, ununuzi, usindikaji na uuzaji wa pamba; na kilimo cha pamba kukosa
msukumo wa kutosha kiuwekezaji.
5. Katika mwaka uliopita, Bodi
ya Pamba ilitekeleza kwa ufanisi, baadhi ya maagizo waliyopewa na Mkutano wa
Wadau wa tarehe 17 – 18 Aprili, 2001 na Wizara. Mambo hayo ni pamoja na:
(a)
Kuzalisha kwa wingi mbegu
mpya ya pamba iliyozalishwa na kituo cha Utafiti cha Ukiriguru inayofaa kwa
ukanda wote wa magharibi. Bodi
ilizalisha kilo 4000 kwa kilimo cha umwagiliaji maji mashambani na msimu huu
wanatarajia kuzalisha 71,150 ambazo zitakidhi nusu ya mahitaji yote ya mbegu
kwa ukanda wa magharibi. Nachukua
nafasi hii kuwapongeza Watafiti wa Ukiriguru kwa kuzalisha mbegu moja mpya
inayofaa kwa ukanda wote wa magharibi ambayo itaondoa tatizo lililosababishwa
na soko huria la kuchanganyika kwa mbegu za pamba. Bodi ya Pamba inapaswa kuandaa mipango mizuri ya kuzalisha mbegu
hiyo kwa wingi katika muda mfupi iwezekanavyo na kuondoa mbegu zote za zamani
ili zisichanganyike na mbegu hii mpya.
(b)
Katika kipindi hiki Bodi
iliandaa na kukamilisha Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Pamba. Kinachotakiwa sasa ni kuandaa programu za
kuutekeleza.
(c)
Katika kipindi hiki Bodi ya
Pamba ilifufua jinari za Mwaya katika
wilaya ya Ulanga, Mandera katika wilaya ya Bagamoyo na Kilosa na iliendesha
kampeni za kuwahimiza wakulima waanzishe au wapanue kilimo cha pamba.
(d)
Aidha, Bodi iliweka mipango
mizuri iliyohakikisha upatikanaji wa madawa ya kuulia wadudu na kupunguza sana
hasara ambayo ingeweza kupatikana.
(e)
Bodi ya Pamba imeanza
kutekeleza majukumu yake vizuri na inastahili pongezi kwa mafanikio yaliyopatikana. Hata hivyo,
bado yapo matatizo mengi ambayo yanahitaji kushughulikiwa haraka.
6. Tatizo la uthibiti hafifu
wa ubora wa pamba inayozalishwa linachangia sana kusababisha pamba yetu ipate
bei ya chini. Tatizo hili linachangiwa
na wakulima wenyewe na kukuzwa sana na ununuzi holela wa pamba unaofanywa na
wanunuzi binafsi. Bodi inapaswa kuweka
utaratibu wa kuthibiti mienendo ya wakulima na wanunuzi wa pamba ili
kuhakikisha kwamba pamba inawekwa katika madaraja sahihi ya ubora na inakuwa
katika hali ya juu ya usafi.
7. Mheshimiwa Waziri
Mkuu, kuna maeneo kadha ambayo
hatujapata mafanikio na kwa kweli hatujayapa umuhimu yanayostahili.
(a)
Uzalishaji wa pamba kwa eka
(tija) bado ni mdogo sana (kg. 250 – 300 tu).
Kwa kutumia samadi na kulitunza shamba vizuri, uzalishaji kwa eka
unaweza kuongezeka kufikia kg. 600 – 700 na kwa kuongeza mbolea za chumvi
chumvi, uzalishaji unaweza kupanda hadi kg. 1000 – 1200 kwa eneo lile
lile. Sheria ya Pamba ya 2001,
inahitaji kusajiliwa kwa wakulima wa pamba na itabidi uongozi katika ngazi
zote, wakiwamo maafisa ugani, wahakikishe kwamba mbinu za kilimo bora
zinafuatwa ili kuongeza uzalishaji na kupunguza uwiano wa gharama za uzalishaji
na mapato.
(b)
Eneo la pili ambalo
halijathibitiwa ni mwenendo mzima wa kuvuna, kusafirisha na kuchambua
pamba. Wakulima wengi hawavuni au kuichambua
pamba na kuiweka kwenye madaraja ya ubora.
Viwanda vya kuchambua pamba navyo vinachambua pamba bila kujali ubora
wake. Kwa kulinda usafi na ubora wa
pamba na kwa kuichambua kwa ‘roller gins’, bei ya kilo moja inaweza
kuongezeka kwa karibu shs. 140/= au USD 15. Ni lazima wakulima, wanunuzi na
wenye viwanda vya kuchambua pamba wazingatie mbinu zote za kuifanya pamba yetu
kuwa bora na wasiofanya hivyo wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
(c)
Tatizo jingine ni lile la
wanunuzi kutokuwalipa wakulima kulingana na ubora wa pamba yao. Tabia hii inawafanya wakulima wasione
umuhimu wa kuichambua pamba na kuipanga kwenye madaraja ya ubora.
(d)
Baadhi ya Viwanda vya nguo
vimeshabinafsishwa na tunatarajia kwamba waliovinunua watachukua hatua za
haraka kuvirudisha kwenye uzalishaji.
Aidha, tunahitaji wawekezaji wengi zaidi ambao watatengeneza nyuzi na
nguo za pamba ili tuuze nguo na nyuzi badala ya pamba ghafi.
8. Bodi ya Pamba peke yake
haina watumishi wa kutosha wa kuiwezesha kutekeleza majukumu yake yote kwa
ufanisi na Wizara yangu haipendekezi kuajiriwa kwa watumishi wengi zaidi. Narudia kuhimiza Bodi zote za mazao
kushirikiana na Serikali za Mitaa kuwapatia watumishi wa kilimo waliopo mafunzo
maalum ya kuwawezesha kusimamia kilimo cha mazao yanayohusika na kuchangia
katika kuwawezesha watumishi hao kutekeleza kazi zinazohusika. Tuwaandae watumishi waliopo ili wawe
mabingwa katika kusimamia kilimo na tuwatumie kikamilifu.
9. Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na matatizo yaliyojitokeza msimu uliopita, matarajio
yetu msimu huu ni mazuri. Hali hii
inatokana na mambo yafuatayo:-
Hali
ya hewa kwa ujumla imekuwa nzuri na ya kuridhisha ijapokuwa katika baadhi ya
maeneo kulikuwepo ukame uliochelewesha upandaji wa zao hili.
Upatikanaji
na usambazaji wa mbegu za kupanda msimu huu haukuwa na matatizo na wakulima
walipata mbegu wakati muafaka.
Upatikanaji
na usambazaji wa madawa ya kuulia wadudu umekuwa mzuri zaidi ingawa bado kuna
matatizo madogo madogo hapa na pale zaidi kuhusiana na mazoea ya wakulima ya
aina fulani tu za madawa ya kuulia wadudu na vinyunyizi vyake.
10. Kutokana na hali ya uzalishaji kuwa nzuri
katika msimu huu, tunatarajia kwamba uzalishaji wa pamba utafikia marobota
325,000 katika msimu wa 2002/2003.
11. Mheshimiwa Waziri Mkuu, baada ya
kusema haya machache, kwa heshima na taadhima nakuomba sasa utufungulie Mkutano wa Pili wa Sekta ya
Pamba nchini.
PAMBA “DHAHABU NYEUPE”
KARIBU SANA.