HOTUBA
YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA MHE. CHARLES N. KEENJA (MB.) KATIKA SHEREHE YA
UZINDUZI WA MBEGU MPYA DAR ES SALAAM, JANUARI 8, 2002
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula,
Mhe. Katibu Mkuu wa Wizara,
Waheshimiwa Wataalam wetu wa Utafiti,
Waheshimiwa Wageni Waalikwa,
Waheshimiwa Wafanyakazi Wote,
Mabibi na Mabwana.
Waheshimiwa Wageni Waalikwa na Watumishi wa Wizara ya Kilimo na Chakula,
napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha kwenye Wizara hii na katika sherehe hii
fupi ya kuzindua mbegu mpya za mahindi na mpunga.
Kwa Wakulima na kwa Wizara hii, kuzalishwa kwa mbegu hizi mpya zenye sifa
bora za kutoa mazao mengi kwa eneo, ukinzani dhidi ya magonjwa na yanayopendwa
na walaji, ni kitendo kinachotupa matumaini kwamba uzalishaji wa chakula nchini
utaongezeka na kuihakikishia familia upatikanaji wa chakula na kuiongezea mapato.
Kwa kifupi, kuzinduliwa kwa mbegu hizi mpya ni kitendo cha maendeleo
katika kilimo. Natanguliza shukrani
na pongezi kwa watafiti wote waliowezesha kuzalishwa kwa mbegu hizi.
Ahsanteni sana.
2.
Mbegu ni moja ya pembejeo muhimu sana katika kilimo.
Kwa bahati mbaya sana, matumizi ya mbegu bora katika nchi hii ni madogo
sana, yanakisiwa kuwa chini ya asilimia kumi tu yakilinganishwa na asilimia 85
Zimbabwe na 62 Kenya. Wakulima wetu
wanatumia mbegu za asili ambazo zinatoa mazao kidogo kwa hekta na huenda zina
ukinzani mdogo. Kuna sababu nyingi
zinazowafanya wakulima waendelee kutegemea mbegu zao za asili badala ya mbegu
bora.
3.
Sababu za Wakulima kutegemea mbegu zao za asili ni pamoja na mbegu bora
kutokupatikana kwa urahisi, kuwa na bei kubwa sana na kutokuwa na baadhi ya sifa
zinazopendelewa na walaji kama ladha, raha na kadhalika.
Hali ya upatikanaji wa mbegu bora hivi sasa ni mbaya kuliko ilivyokuwa
kabla ya kuanzishwa kwa soko huria. Shirika
la TANSEED ambalo lilikuwa na wajibu wa kuzalisha na kusambaza mbegu bora na
zilizodhibitishwa liko katika hali mbaya kifedha na haliwezi kutekeleza majukumu
yake hata kwa kiwango kidogo. Mfumo wa kuzalisha na kusambaza mbegu bora kwa hiyo,
umevurugika na Wizara ya Kilimo na Chakula iko mbioni kubuni mfumo mpya ambao
utategemea zaidi ushirikiano kati ya vituo vya utafiti, ambavyo vitazalisha
mbegu ya watafiti, mashamba ya mbegu ambayo yatazalisha mbegu za msingi (foundation
seed) na wakulima binafsi, ambao watasimamiwa kuzalisha mbegu bora
zilizothibitishwa (certified seed). Wote wanaohusika wanaagizwa
kuharakisha kazi hii ili ikamilike mapema, kwa vyovyote vile, kabla ya mwisho wa
mwezi Machi, 2002.
4.
Mbegu tunazozindua leo zina sifa bora ambazo amezieleza Katibu Mkuu na
ambazo nitazirudia baadaye kidogo. Tumekuwa
tukiziona mbegu hizi katika vituo vya utafiti na katika maonyesho mbali mbali
yakiwamo yale ya Nane Nane 2001, na ya Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika
Dodoma mwaka jana . Tunalofanya leo
ni kuziondoa mbegu hizo kutoka kuwa za maonyesho na kuzifikisha katika hatua
ambapo zitazalishwa kwa wingi na kusambazwa kwa wakulima.
5.
Ningependa kurudia hapa kwamba Wizara ya Kilimo na Chakula inachukua
hatua za makusudi kuhakikisha kwamba mbegu bora zinapatikana kwa wingi na kwa
bei ambazo mkulima atazimudu. Kwa
muda sasa, wakulima wamekuwa wakiwezeshwa kuzalisha mbegu bora kwenye vijiji
vyao chini ya mpango wa Agricultural Sector Programme Support
unaohisaniwa na DANIDA. Utaratibu
huo utaendelezwa na kupanuliwa. Sambamba
na mpango wa wakulima kuzalisha mbegu vijijini, tunao wakulima wa kati na
wakubwa nao waanzishe kilimo cha mbegu bora na tunawaahidi mbegu za msingi (foundation
seed) na ushauri wa kitaalam ili kuwawezesha kufanya kazi hii kwa misingi
sahihi na kwa ufanisi.
6.
Mashamba ya mbegu yaliyoko Arusha, Ilonga - Kilosa, Msimba - Kilosa,
Mwele - Tanga, Kilangali - Kilosa, Dabaga - Iringa, yataendelea kutumiwa
kuzalisha mbegu za msingi na kwa sababu hiyo, hayatabinafsishwa au kuuzwa.
Mashamba hayo yatakuwa sehemu muhimu ya mfumo wa uzalishaji mbegu ambao
utaanzia kwenye vituo vya utafiti, mashamba ya mbegu na kuishia na uzalishaji wa
mbegu zilizothibitishwa ambao utafanywa na wakulima vijijini, shule za msingi na
sekondari, NGO, vikundi vya dini na wakulima wa kati na wakubwa wa mbegu.
Uzinduzi wa mbegu hizi mpya leo, ni sehemu muhimu ya mfumo huo wa
kuzalisha mbegu nchini.
7.
Mbegu bora ni pembejeo muhimu ya kilimo lakini peke yake, mbegu bora
haitamhakikishia mkulima mazao mengi. Tunahitaji
kuwa na utaratibu mzuri wa kumpatia mkulima mahitaji yake ya mbolea na madawa ya
kuulia wadudu kwa wingi, kwa wakati na kwa utaratibu utakaomwezesha kuyapata kwa
urahisi karibu na shamba lake. Kwa
wakati huu, mfumo wa kuingiza mbolea na madawa nchini, kama ule wa mbegu,
umevurugika na unategemea soko huria. Tumeanza
kuweka utaratibu wa kushauriana mara kwa mara na waagizaji na wasambazaji wa
mbolea na madawa ili kuhakikisha kwamba wanaingiza nchini pembejeo hizo za
kutosha na wanazifikisha mikoani. Aidha,
tunahimiza kusambazwa kwa mbolea ya Minjingu Phosphate ambayo ina sifa bora sana
za kuipatia mimea mahitaji yake ya virutubisho na wakati huo huo kupunguza tindi
kali kwenye udongo. Wizara
inashirikiana na sekta binafsi kuweka utaratibu wa uhakika wa kuingiza mbolea na
madawa nchini na kuyasambaza.
8.
Tatizo kubwa sana linalotukabili ni uwezo mdogo wa wakulima wa kununua
mahitaji yao ya mbegu, mbolea na madawa kwa fedha taslimu.
Tunahitaji utaratibu utakaomwezesha mkulima kupata mahitaji yake ya
pembejeo kwa mikopo yenye masharti nafuu. Aidha,
kadri uchumi wetu utakavyozidi kukua, itabidi tuangalie jinsi Serikali
itakavyoweza kumsaidia kubeba mzigo wa gharama hizo.
Kwa ufupi, mfumo wote wa kilimo unatazamwa upya kwa lengo la kuwezesha
kukua kwa uzalishaji, kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi na kuongeza
mchango wa kilimo katika uchumi wa Taifa.
9.
Ili kilimo chetu ambacho kinategemea wakulima wadogo wadogo wanaoishi
vijijini kikue, ni sharti mipango ya kilimo ya vijijji iwe inaandaliwa na
kusimamiwa kwa umakini kuliko ilivyo sasa, vinginevyo vijiji vyetu vitakuwa
maskani yanayolea umaskini tu. Vijiji
ni sharti view vituo vya uzalishaji katika kilimo, viwanda vidogo vya kusindika
mazao na kutengeneza mahitaji ya wana vijiji na kadhalika.
Mipango ya kilimo ya vijiji ikiandaliwa vizuri, ndipo wakulima
watakapoweza kufaidika na mbegu bora, matumizi ya mbolea na madawa n.k.
10.
Ni muhimu sana kwa wakulima kuanzisha na kujiunga na vyama vya ushirika
na vyama vya kuweka na kukopa. Ipo
mifano mingi ya mafanikio ambayo wananchi wamepata kwa kujiunga na vyama vya
uzalishaji wa mazao na vya kuweka na kukopa.
11.
Pamoja na kuzindua mbegu mpya, mwaka huu Wizara itaanza kuzalisha kwa
wingi na kusambaza aina nane za mbegu kama ifuatavyo:
1.
PAMBA (uk. 91) kuzalishwa kwa wingi ili
ziweze kutosheleza mahitaji ukanda wote wa Magharibi.
2.
MTAMA (PATO na MACIA), kuzalishwa na
vikundi vya wakulima Mikoa ya Dodoma na Singida
3.
MAHINDI (KILIMA ST) Kuzalishwa na vikundi
vya wakulima mikoa ya Mara na Mwanza chini ya usimamizi wa Kituo cha Ukiriguru
tani 300 zinatarajiwa kuzalishwa.
UYOLE HYBRID 615 mbegu hii itazalishwa tena chini ya usimamizi wa Kituo cha Uyole. Tani 200 zinatarajiwa kuzalishwa.
4.
MBAAZI
KOMBOA Tani 5 za mbegu hii zitazalishwa na vikundi vya wakulima
mkoani Morogoro chini ya usimamizi wa kituo cha Ilonga.
5.
MAHARAGE
(LYAMUNGU 90, UYOLE 98). Vikundi vya Wakulima vitazalisha mbegu hizi
kiasi cha tani 20 kando za Kaskazini na Nyanda za Juu kusini chini ya usimamizi
wa vituo vya Selian na Uyole.
6.
Mahindi yenye proteini nyingi (High Protein Quality Maize) ambayo
itazalishwa Arusha.
7.
Low nitrogen draught tolerant Maize nayo yatazalishwa kwenye shamba la
mbegu la Arusha.
11. Baada ya
maelezo hayo ya utangulizi sasa natamka rasmi kuzinduliwa kwa mbegu zifuatazo:
MBEGU
MPYA ZILIZOTOLEWA NA WATAFITI WA WIZARA MWAKA WA 2001
MAHINDI
(1).
Uyole Hybrid 615 (UH 615)
KITUO:
ARI Uyole
KIONGOZI
WA UTAFITI:- DR. NICK LYIMO
Sifa:
Inavumilia ugonjwa wa ukungu wa Mahindi, Grey Leaf Spot (GLS) na kutoa
mavuno mengi ya tani 8 10 kwa hekta
(2).
LISHE 1)
(3).
LISHE 2)
- Quality Protein Maize (QPM)
KITUO:
ARI SELIAN
KIONGOZI
WA UTAFITI:- DR. ZUBEDA MDURUMA
SIFA:
Zina virutubisho bora zaidi vya lishe vitakavyoweza kupunguza utapiamlo
nchini.
(4).
SITUKA 1
(5).
SITUKA 2
KITUO:
ARI SELIAN
KIONGOZI
WA UTAFITI: DR. ZUBEDA MDURUMA
SIFA:
Z|inavumilia ukame na pia husitawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba
ndogo na kuweza kutoa mavuno ya tani 3-4 kwa hekta
(6).
KILIMA ST
KITUO:
ARI SELIAN
KIONGOZI
WA UTAFITI: DR. ZUBEDA MDURUMA
SIFA:
Hustawi kwenye mazingira mengi tofauti na kustahimili ugonjwa wa melea ya
mahindi (streak virus). In uwezo wa
kutoa mavuno tani 6 kwa hekta.
(7).
TMV 1 ST
KITUO:
ARI SELIAN
KIONGOZI
WA UTAFITI: DR. ZUBEDA MDURUMA
SIFA:
Inastahimili sana ugonjwa wa melea ya mahindi (maize streak virus) na
kutoa mavuno ya tani 5 6 kwa hekta.
MPUNGA
(8).
TXD 85
(9).
TXD 88
KITUO:
ARI DAKAWA/ ARI IFAKARA
KIONGOZI
WA UTAFITI:
DR. Z. KANYEKA/MR. MSOMBA
SIFA:
Ni mbegu za kwanza kutolewa nchini zilizo na uwezo wa kutoa mavuno mengi
kwa ekari (tani 6-8) na pia kuwa na ladha nzuri.
12.
Baada ya kufanya hivyo napenda niungane na Katibu Mkuu kuwapongeza
watafiti wote mliofanyakazi hii chini ya mazingira ambayo mara nyingi yalikuwa
magumu. Mchango wenu katika
kuchangia kupunguza umasikini nchini unatambuliwa.
Wizara itajitahidi kuwaongezea uwezo na kuboresha mazingira yenu ya kazi
kadi uwezo utakavyoruhusu.
13.
Katika miaka hii, tumeona bei za mazao yetu ya biashara zikiporomoka kwa
viwango vya kutisha. Vituo vyetu vya Utafiti na Watafiti wetu wanakabiliwa na
changamoto la kuzalisha mbegu za mazao yatakayolimwa badala ya yale ambayo bei
zake zimeshuka sana. Kituo cha
Utafiti cha Katrin kimeagizwa kuzamia katika kukusanya mbegu za aina nyingi ya spices
kama uwezekano na kufanya utafiti
wa njia bora za kuzizalisha kwa wingi. Tunahitaji
aina nyingine nyingi za mbegu za mazao mapya na kazi hii ni ya haraka sana.
Ianze mara moja bila kusubiri.
14.
Mwisho, nawatakia heri na fanaka ya mwaka mpya, mwaka wa 2002.
Kwetu katika wizara ya Kilimo na Chakula, huu ni mwaka wa kazi nyingi na
ngumu za kufafanua matatizo yanayokabili kilimo na kubuni njia za kuyapatia
ufumbuzi. Mafanikio yetu yatapimwa
kwa viwango vya kuongezeka kwa uzalishaji, vya kupungua kwa umaskini na mchango
katika Uchumi wa Taifa. Tunatambua
kwamba shughuli za kilimo zinahusu wakulima na taasisi nyingi na Wizara na idara
ya Serikali na Washiriki wetu katika maendeleo.
Aidha, kilimo ni shughuli inayoongozwa na sekta ya watu binafsi.
Tutashirikiana na kuwashirikisha washikadau wote wa kilimo katika kupanga
na kutekeleza mipango ya maendeleo ya kilimo nchini.
Tungependa kuona mapinduzi katika kilimo chetu na tunaamini kwamba uwezo
tunao na nia tunayo. Tunachohitaji ni kuweka mifumo itakayomwezesha mkulima
kupata mahitaji yake ya kilimo ya kuyafikia masoko yenye bei nzuri.