Skip to main content
Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Vijana 812 waliochaguliwa kujiunga katika programu ya BBT-YIA awamu ya kwanza watajwa

Wizara ya Kilimo leo Februari 23, 2023 Jijini Dodoma imetangaza awamu ya kwanza ya majina 812 ya vijana waliochaguliwa kujiunga katika programu ya Building Better Tomorrow: Youth Initiative in Agribusiness (BBT-YIA)Serikali kupitia programu hii itawawezesha vijana kushiriki kilimo biashara kupitia mashamba ya pamoja (block farms).

Awali, Wizara ilitoa tangazo kwa Umma kwa ajili ya vijana kuwasilisha maombi kupitia tovuti www.bbt.kilimo.go.tzili kujiunga na mafunzo ya kilimo biashara katika vituo Atamizi. Dirisha la maombi lilifunguliwa tarehe 10 Januari, 2023 na kufungwa tarehe 30 Januari, 2023. Hadi dirisha la maombi lilipofungwa,    jumla ya maombi yote yaliyopokelewa ni 20,227 kati yao Wanawake ni 4,722 sawa na asilimia 23.34.

Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa kuwa na waombaji wengi wapatao 2,931 sawa na asilimia 14.49 ya maombi yote na Mkoa wenye waombaji wachache ni Lindi ambapo jumla ya maombi 109 yalipokelewa sawa na asilimia 0.54. Kwa upande wa Halmashauri,  Jiji la Dodoma limeongoza kwa kuwa na waombaji wengi wapatao 1,800 sawa na asilimia 8.89 ya maombi yote na Halmashauri yenye waombaji wachache zaidi ni Nyasa ambayo ina jumla ya waombaji 06 sawa na asilimia 0.03 ya maombi yote.

Wizara imekamilisha taratibu za udahili na kuwapata vijana 812 watakaoshiriki mafunzo kwa awamu ya kwanza. Kati yao Wanawake ni 282 sawa na asilimia 34.73 na wanaume 530 sawa na asilimia 65.27 ya waliochaguliwa. 

Vijana waliochaguliwa watapata mafunzo kwa kipindi cha miezi minne katika vituo 15 vilivyoandaliwa na watatakiwa kuripoti katika vituo watakavyopangiwa tarehe 17 machi, 2023 bila kukosa.  Wakati wote wa mafunzo, Serikali itagharamia Malazi, Chakula na gharama za mafunzo.  Aidha vijana watatakiwa kujigharamia usafiri na mahitaji binafsi. Vituo vya kuripoti kwa waliochaguliwa vitatangazwa kabla ya tarehe 10 Machi, 2023. 

Orodha ya waliochaguliwa inapatikana kupitia kiunganishi (Orodha ya waliochaguliwa awamu ya kwanza) na katika kurasa za mitandao ya kijamii za Wizara ya Kilimo. 

Imetolewa na;

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

WIZARA YA KILIMO