Skip to main content
Habari na Matukio

Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Makambako yanunua Mahindi zaidi ya tani elfu 16

Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Makambako yanunua Mahindi zaidi ya tani elfu 16 katika msimu wa kilimo wa 2016/2017

Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Makambako, Bwana Bright Mollel amesema Kanda ya Makambako imefanikiwa kununua shehena ya mahindi zaidi ya tani elfu 16, akiongea mbele ya wanahabari, hivi karibuni wakati wa mahojiano maalum ofisini kwake.

Bwana Mollel amesema Kanda ya Makambako ilikuwa na lengo la kununua mahindi kiasi cha tani elfu 20 katika Mkoa wa Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe ambapo katika utekelezaji wa agizo hilo, kwenye msimu wa kilimo wa 2016/2017. Wakala Kanda ya Makambako imefanikiwa kununua kiasi cha tani 16,279.298 ambapo ni sawa na asilimia 81.2 ya lengo.

Bwana Mollel aliongeza kuwa kiasi kikubwa cha shehena ya mahindi kilinunuliwa kutoka katika Mkoa wa Njombe ambapo tani 10,478,696 zilinunuliwa na kuongeza kuwa Vituo vya ununuzi vya Shaurimoyo na Mlangali vilivyo katika Wilaya ya Ludewa viliongoza kwa ununuzi wa tani 3,268.441 na tani 2167.537 za mahindi kutoka katika kila Kituo.

Kwa upande wa Mkoa wa Songwe Kituo cha ununuzi cha Ileje kilichopo Wilaya ya Ileje na kile cha Ndalambo kilicho katika Wilaya ya Momba viliongoza kwa kuwa na shehena kubwa ya mahindi ambapo kiasi cha mahindi tani 1,346.379 na tani 829.792 zilinunuliwa na Wakala.

Bwana Mollel aliongeza kuwa Kanda ya Makambako ipo katika hatua ya mwisho ya kuongeza uwezo wake wa kuhifadhi mazao kabla ya msimu mpya wa ununuzi haujanza na ameongeza kuwa kwa kutumia sehemu ya fedha za ndani, Kanda imeanza kujenga ghala lenye uwezo wa kuhifadhi shehena ya mazao kiasi cha tani 5,000 na kuongeza kuwa ujenzi unatarajiwa kukamilika kabla ya msiku ujao wa ununuzi kuanza.

Bwana Mollel aliongeza kuwa ujenzi wa ghala hilo umeanza katika kiwanja kilichopo ndani ya maghala ya Mbozi katika Mkoa wa Songwe.

Aidha, Bwana Mollel alikaririwa akisema “lengo la Serikali ni kuhakikisha taifa linajitosheleza kwa chakula na ikiwezekana, Tanzania iwe ghala la chakula katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi shehena kubwa ya chakula, tutawahakikishia wakulima wa Tanzania kununua mazao yao na kuwa na ziada ya kutosha”.

Bwana Mollel aliongeza kuwa Kanda ya Makambako itafanikiwa mara dufu kuongeza uwezo wa kuhifadhi shehena kubwa ya chakula mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa maghala makubwa (silos) ambapo kwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Poland, ambapo Mkandarasi kutoka nchini Poland ameshapatikana na ujenzi unatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa.

Bwana Mollel alidokeza kuwa ujenzi huo wa maghala makubwa na ya kisasa (silos) utakapokamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi wa Wakala Kanda ya Makambako mara dufu kutoka uwezo wa sasa wa tani elfu 34.