Skip to main content
Habari na Matukio

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Amesema Hapendi Kuona Tasnia ya Sukari Ikikosa Mwelekeo

Mhe. Eng. Christopher Kajoro Chiza (Mb) Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika ameonya kuwa kuwa Serikali haitapenda kuona Tasinia ya Sukari ikikosa mweleleo kutokana na matakwa ya kundi fulani. Alisisitiza kuwa, Tasnia ya sukari ni moja ya tasnia kubwa nchini ikijumuisha wadau muhimu wakiwamo walaji, wakulima, wafanyabiashara na wazalishaji. Kila mdau katika jumuisho hili ana maslahi ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kukinzana na ya mdau mwenzake. Mkulima angependa kuona anauza miwa yake kwa bei ya juu, hali kadhalika mzalishaji kuuza sukari anayozalisha kwa bei yenye faida ya kutosha. Aidha mfanyabiashara angependa kupata faida maradufu na panapokuwa na mwanya kuingiza sukari kutoka nje kwa njia sizizo halali. Lakini kwa upande mwingine mlaji naye angependa kununua sukari kwa bei nafuu.

Serikali haipo tayari kuona tasnia kubwa na muhimu kama hii ya sukari ikipoteza mwelekeo, aidha ingependa kuwepo kwa mazingira mazuri (win - win situation) kwa kila mdau. Kwa maana hiyo nimeona ni jambo jema na muhimu sana kuwakutanisha ninyi wadau ili tuweze kujadili kwa pamoja changamoto zilizopo mbele yetu juu ya sekta hii. Ni matarajio yangu kwamba, mkutano huu utaweka misingi ya kufikia utatuzi wa chamngamoto hizi kwa manufaa ya pande zote

Mhe. Waziri ameyasema hayo katika mkutano wa Wadau wa Sukari uliofanyika Mjini Morogoro mwanzoni wa mwezi Januari

Akitoa picha halisi ya uzalishaji na mahitaji ya sukari hapa nchini Waziri Chiza alisema kuwa, Wakati viwanda vyetu vinabinafsishwa vilikuwa vinazalisha wastani wa tani 120,000 kwa mwaka. Sasa uzalishaji umefikia wastani wa tani 300,000 kwa mwaka.

Aidha uzalishaji wa miwa (siyo sukari) katika mashamba ya wakulima wadogo nao umeongezeka kwa asilimia 61 (hii ni kutoka wastani wa uzalishaji wa tani 439,122 hadi tani 705,176 kwa mwaka). Uzalishaji katika mashamba ya wenye viwanda umeongezeka kutoka wastani wa tani 1,083,738 na kufikia tani 2,229,274 kwa mwaka (ongezeko la asilimia 105).

Pamoja na mafanikio haya bado tasnia ya sukari imegubikwa na changamoto mbali mbali kubwa zaidi ikiwa uzalishaji usiokidhi mahitaji. Mahitaji yetu ni wastani wa tani 590,000 za sukari kwa matumizi ya kawaida na ya viwandani. Viwanda vya sukari nchini huzalisha takribani asilimia sabini tano (75%) ya mahitaji ya sukari ya matumizi ya kawaida. Wastani wa tani 290,000 ni nakisi inayojazwa na uagizaji sukari kutoka nje. Nakisi hii inajumuisha sukari ya matumizi ya kawaida (gap sugar) ya wastani wa tani 120,000 na sukari ya matumizi ya viwandani ya wastani wa tani 170,000 kwa mwaka. Kiasi chote cha sukari ya matumizi ya viwandani kinaingizwa nchini kutoka nje. Aidha uagizaji wa sukari ya matumizi ya kawaida unategemea hali halisi ya soko kwa kipindi husika na kwa hiyo uagizaji halisi unaweza kuwa juu au chini ya nakisi hiyo. Hata hivyo, Kamati ya Ufundi ya Ushauri ya Uagizaji Sukari iliyokutana tarehe 24/12/2013 kujadili hali ya sukari nchini imependekeza kuwa mwaka huu 2013/2014 kusiwe na uagizaji wa sukari kwa sababu kiasi tha tani 257,000 kitapatikana kwa matumizi ya kawaida kuanzia sasa hadi mwishoni mwa 2013/2014.