Skip to main content
Habari na Matukio

ASILIMIA 80 YA PAMBA IMESHAUZWA NJE-MHE.BASHE

Dodoma.

Naibu Waziri wa Kilimo Husein Bashe  amefanya mazungumzo  na wadau wa tasnia ya pamba  ili kufanya mapitio ya ununuzi  na uuzaji  kwa msimu uliopita na kujiandaa  kwa msimu ujao.

Aidha kikao hicho kimehudhuriwa na Taasisi za fedha,bodi ya pamba pamoja na wanunuzi wa pamba  katika kupata mwenendo mzima  wa pamba kwa msimu uliopita.

Mhe Bashe  amesema Serikali ilitoa maelekezo katika msimu wa pamba kuwa  pamba yote inunuliwe na sekta binafsi iwapatie fedha kwa ajili ya kununua  na  kulikuwa na  mapitio kujua hali ikoje na wameuza kiasi gani  nje  mpaka sasa na kwa takwimu za haraka ni kwamba karibu asilimia 80 imeshauzwa nje  huku msimu mpya umeshaanza .

“ Wakulima safari hii waligaiwa mbegu kwa mkopo wote kwa hiyo tulikuwa tunajaribu kuangalia kwa ajili ya majadiliano ya awali kufanya mapitio ya msimu uliopita vilevile kujiandaa kwa msimu ujao”amesisitiza Mhe.Bashe

Hata hivyo ameongeza kuwa safari hii pamba ilinunuliwa chini ya usimamizi wa serikali  na sekta  ya fedha ambapo kulikuwa na makubaliano kati ya serikali na wanunuzi,msimamizi ambaye ni Benki kuu .

‘’Hivyo kikao hiki ni kwa ajili ya kupitia kwa ufupi, kuangalia  na kupeana muda  mpaka wiki ijayo kila mnunuzi alete taarifa  ameuza kwa shilingi  ngapi,gharama zake ni shilingi  ngapi  ili  waone ni namna  gani ahadi za Serikali zinaenda kwenye utekelezaji’’ Amesema Mhe.Bashe

 Aidha  amesema kuwa jambo jingine muhimu katika majadiliano ni kukubaliana kwamba msimu unaokuja malipo yote yatakuwa kupitiaa benki na  hakutakuwa na mambo yakulipana cash.

 

“Changamoto ambayo tunayo kwa sasa ni kwamba wanunuzi wanadaiwa fedha za  AMCOS,lakini AMCOS zimetumia fedha za kuwalipa malipo ya wakulima  kwa ajili ya kulipia shughuli za uendeshaji  kwa hiyo unakuta kwenye baadhi ya maeneo kuna wakulima wachache wanadai “Ameongeza kusema

 Hata hivyo  Bashe  amesema  wanakusanya hizo takwimu kupitia bodi halafu wakishamaliza hii ripoti kupitia kikosi kazi  ambacho kitakuwa kinaongozwa na Mwenyekiti wa  Mabenki kwamba kabla ya tarehe 31 januari  kuwe tayari na taarifa rasmi .

 Aidha amewaomba  wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya  kutochukua hatua za kutumia nguvu  katika kukusanya fedha kutoka kwa wafanya biashara kwa sababu kutakuwa na kikao ambacho kitatoa maamuzi ya pamoja  ya malipo  ya shilingi 33 kwa ajili ya  AMCOS.

Pia amesema jumla ya kampuni ambazo zimenunua pamba mwaka huu ni 23 kutoka kwa wakulima jumla ya tani 350,000 ambazo zimenunuliwa kiujumla ambazo ni kilo milioni 350 na wafanyabiashara wa Tanzania  wengi wamebaki na kiwango kisichozidi asilimia kumi mpaka sasa.

 Naye Mkurugenzi  Mkuu wa CRDB Abdumahjid   Isekelaa amesema kuwa amefurahishwa na ushirikianao ambao wizara inafanya kati ya taasisi za fedha na wanunuzi wa pamba na kusema kuwa mabenki yalishiriki kwa kina sana  msimu uliopita  kwenye kukopesha  ambapo wamiliki wa mabenki wameshiriki katika kikao hiki ili  kuangalia mwenendo wa ununuzi wa pamba ulivyokwenda. 

 Mwisho.