Skip to main content
Habari na Matukio

DKT. TIZEBA AFUKUZA KAZI WATATU, ATOA ONYO KWA WATATU

Waziri wa Kilimo, Mhe. Dkt. Charles Tizeba amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Methew Mtigumwe  kuwafukuza kazi Maafisa watatu wa Idara ya Maendeleo ya Mazao katika Sehemu ya Pembejeo ambao wamebainika kuhusika moja kwa moja na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Akizungumza na vyombo vya habari katika Ukumbi wa Lenny Mjini Geita Mhe. Tizeba alisema kuwa kufukuzwa kazi kunajili kutokana na ukosefu wa umakini na usimamizi mzuri wa sheria ya ununuzi wa Umma ikiwemo kusababisha kuchapishwa kwa vocha za pembejeo zenye thamani ya Tshs 78,054,970,000 ambazo ni zaidi ya bajeti halisi iliyotengwa kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo kwa kiasi cha Tshs 42,587,419,200

Watumishi waliofukuzwa kazi ni Bwana Shenal S. Nyoni aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Pembejeo, aliyekuwa Afisa Kilimo Daraja la I, Bwana Michael G. Mayabu na Bwana Franks F. Kamhabwa.

Waziri Tizeba ametumia mamlaka hayo mara baada ya kupitia Taarifa ya Waraka wa Mkakati wa Utekelezaji na Usimamizi wa utoaji wa Ruzuku za Pembejeo za Kilimo kwa Wakulima kwa kutumia Mfumo wa Vocha wa mwaka 2015/2016 ambapo pamoja na mambo mengine uliainisha utaratibu wa usimamizi wa zoezi la utopaji wa ruzuku ambao ulilenga kuleta ufanisi katika utekelezaji wake.

Wakati wa utekelezaji wa zoezi la usimamizi wa Mpango wa Ruzuku za Pembejeo katika Msimu wa mwaka 2014/2015 - 2015/2016 kulijitokeza tuhuma mbalimbali zilizohusu ukiukwaji wa taratibu uliofanywa na Watumishi wa Serikali za Mitaa zilizohusika kwenye Mpango wa Ruzuku, Watumishi hao walituhumiwa kushirikiana na Mawakala waliokuwa wamepewa dhamana ya kusambaza pembejeo katika kuhujumu mpango huo serikalini.

Ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo pamoja na uhakiki uliofanywa na Wizara ya Fedha na Mipango kuthibitisha uhalali wa madeni ya Mawakala, mwezi Aprili, 2017 Wizara ya Kilimo ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwasimamisha kazi watumishi watano wa Idara ya Maendeleo ya Mazao, Sehemu ya Pembejeo waliohusika kusimamia mpango wa Ruzuku za Pembejeo za kilimo.

Aidha, Mwezi Mei, 2017 Wizara ya Kilimo iliunda Kamati ya uchunguzi ili kuchunguza tuhuma zilizowahusu Watumishi hao waliosimamishwa kazi.

Katika hatua nyingine Mhe. Dkt. Tizeba amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Methew Mtigumwe kuwasimamisha kazi Watumishi wengine watatu ambao ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao Bwana Twahir S. Nzallawahe, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi Bwana Burhan A. Shaban, na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Pembejeo, Bwana Canuth Komba.

Zaidi ya shilingi 29,977,114,700 zingepotea kama umakini usingekuwa mkubwa katika uhakiki kwani katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 serikali ilitenga kiasi cha shilingi 35,467,550,800 kwa ajili ya pembejeo za kilimo na mara baada ya zoezi la utoaji ruzuku ilibainika kuwa deni lililowasilishwa serikalini na mawakala ilikuwa ni kiasi cha shilingi 65,444,665,500.

Sambamba na hayo Mhe. Waziri Tizeba aliviomba vyombo vya dola kuchunguza zaidi na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya Watumishi na watu wote waliohusika katika ngazi za Halmashauri na Mawakala wote waliofanya udanganyifu huo kwa lengo la kuisababishia Serikali hasara.