Skip to main content
Habari na Matukio

MGUMBA AITAKA AGITF KUJITANGAZA

Dodoma.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Omari  Mgumba ameutaka Mfuko wa pembejeo wa Taifa (AGITF)  kujitangaza ili  wakulima waweze kuja kukopa pembejeo hizo kwa ajili ya kuinua kilimo chao katika kuendeleza mnyororo wa thamani.

Mhe Mgumba aliyasema hayo mara baada ya kukutana na watumishi wa Taasisi hiyo leo tarehe (15.1.2020 ) na kuwaelekeza  kuandika maandiko yenye tija kwa wananchi ili Serikali ione umuhimu wa kuwapatia fedha na kuwa na uwezo wa kukopesha watu wengi zaidi.

“Mfuko huu haufahamiki kwa watanzania walio wengi ,matokeo yake wanaoufahamu ni wale wale wajanja wajanja,ni wale wanaojua kucheza na pesa za umma na wengi ndio waliofanikiwa kuupata”alikaririwa akisema

Aidha,Mhe Mgumba alisema  kwamba wale ambao ni wahitaji wa kweli hawaufahamu mfuko huo hivyo ni vyema kujitangaza ili walengwa waweze kunufaika na pembejeo hizo za kilimo  kwani tunapofanya hivyo tunakuza kipato cha mkulima

Hata hivyo Mhe.Mgumba ameitaka sheria ya mkopo ifanyiwe marekebisho kwani iliyopo sasa ina mapungufu mengi  ikiwemo kutumika kwa hati za kimila. Hiyo ni changamoto  kubwa  kwani ukimkopesha mtu kwa hati ya kimila mali yake haiwezi kuuzika  na  inasema kuwa mnunuzi lazima atoke kwenye kijiji kile kile.

“Lazima tufanye maboresho ya kisheria ili kwamba sheria yetu ikidhi  mahitaji ya sasa ili dhamana itoe ruhusa ya  nyumba au shamba kununuliwa na mtu yoyote yule iwe ndani au nje ya nchi.” Alisema Mgumba

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa pembejeo wa Taifa Festo Modestus Mhimba amesema kwamba tangu mwaka 1994 hadi 2018,mfuko umepokea jumla ya shilingi 34,880,111,317.03 na umefanikiwa kutoa mikopo 3,590 yenye thamani ya jumla ya shilingi 82,772,251,770.00 na kusema kwamba ongezeko hilo la fedha limetokana na marejesho ya mikopo na riba.

Mkurugenzi huyo ameendelea kusema kwamba mfuko haujawahi kujitangaza kimkakati kwa kuhofia kupokea maombi ya mikopo yanayozidi uwezo wa kuyahudumia. Licha ya hivyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 mfuko ulijipanga kufanya marejesho ya jumla ya shilingi 5,508,2091,668.00 na kutoa mikopo 250 ya jumla ya shilingi 4,119,000,000.00.

Hata hivyo mpaka Desemba 2019 mfuko umepata marejesho ya jumla ya shilingi 1,295,225,943.12 na umetoa mikopo 93 ya jumla ya shilingi 836,090,000.00.Aidha mfuko umepokea fedha kutoka hazina jumla ya shilingi 336,468,600.00 kati ya 524,479,818.00.

Mwisho.