Skip to main content
Habari na Matukio

Mhandisi Methew Mtigumwe: Maonesho ya nanenane ni taswira chanya kwa wakulima

Maadhimisho ya Sherehe za wakulima maarufu kama Nane Nane zimetajwa kuwa ni darasa huru kwa wakulima, wadau wa kilimo na wananchi kwa ujumla kwani zinatoa nafasi kwao kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo kilimo chenye tija, Ufugaji wa kisasa na Uvuvi wenye tija pasina kuharibu rasilimali za Serikali.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mhandisi Methew J. Mtigumwe wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.

Amesema Serikali inatambua kadhia inayowakabili Wakulima nchini ikiwemo pembejeo feki ambazo wakulima wanauziwa, hivyo kupata hasara ikiwamo mazao kidogo na hafifu tofauti na kusudio lao la kujipatia mazao mengi ya biashara na chakula jambo ambalo inalifanyia kazi ili kukabiliana nalo kwa haraka.

Maonyesho haya Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi yatawasaidia wakulima kupata elimu ya pembejeo halisi ikiwamo mbegu, dawa (viuatilifu), mbolea kutoka kwa mashirika husika yanayozalisha pembejeo mbali mbali, ili kuwasaidia kuepuka kununua pembejeo feki ambazo huwasababishia hasara na kuwakatisha tamaa.

Sherehe hizi huambatana na Maonyesho ya bidhaa za kilimo yanayofanywa na Wakulima na Mashirika mbalimbali yanayojihusisha na masuala ya kilimo, lengo likiwa ni kutangaza shughuli zao, kubadilishana uzoefu na wataalam wa kilimo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Mhandisi Mtigumwe amesema kupitia Maadhisho haya Wakulima wadogo ambao ni wengi ukilinganisha na wakulima wakubwa watajifunza mbinu mpya za kitaalamu za kilimo zinazoendana na wakati uliopo ili kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia na ya tabianchi na hatmae walime waweze kilimo cha kisasa kwa ajili ya kuongeza tija na uzalishaji.

Mhandisi Mtigumwe amesema kwa muda mrefu Wakulima wamekuwa wakilima kilimo cha mazoea ambacho hakizingatii kanuni za kitaalam, jambo lililowasababisha kukata tamaa na kuona kuwa kilimo hakilipi kutokana na mbinu duni ambazo wamekuwa wakizitumia.

Ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi inajipambanua zaidi ili kuwa kwamua Wakulima nchini waondokane na kilimo cha kubahatisha cha kutegemea mvua na badala yake wajikite katika kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha uhakika, kinachoweza kuyabadilisha maisha yao kiuchumi kutokana na mazao mengi watakayopata.

"Natambua kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanategemea Sekta ya Kilimo kama ajira yao sehemu kubwa ya kilimo ni cha Wakulima wadogo wadogo ambao mashamba yao yana ukubwa wa hekta 0.9 na hekta 3.0 kwa kila moja, Karibu asilimia 70 ya ardhi ya kilimo na mazao inalimwa kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 hutumia maksai na asilimia 10 hutumia trekta hivyo kama Wizara tutajitahidi kadri iwezekanavyo kuwakwamua Wananchi ili kuondokana na uduni katika mavuno" Akaririwa Mhandisi Mtigumwe.

Mhandisi Mtigumwe ameongeza kuwa katika maonesho hayo anatarajia Wakulima watajifunza mbinu bora na za kisasa za kilimo zitakazowawezesha kupata mazao mengi na kuinua kipato chao.

Aidha ametoa wito kwa Wakulima na Mashirika kujitokeza katika Maonesho hayo kwa sababu watapata fursa ya kujifunza mambo mengi na kubadilishana uzoefu na wataalam mbalimbali wa kilimo.