Skip to main content
Habari na Matukio

NAIBU WAZIRI MHE. HUSSEN BASHE ATEMBELEA SHAMBA LA WAKALA WA MBEGU ARUSHA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, akiwa ziarani mkoani Arusha leo tarehe 01/07/2020 amefanya ziara ya kikazi katika Shamba la Wakala wa Mbegu Bora za Kilimo nchini – ASA lililopo Ngaramtoni  mkoani hapa akitokea Monduli alipokua akizungumza na wakulima na wanunuzi wa zao la Shayiri ambapo aliwahakikishia soko wakulima hao na kuwataka kununua Mbegu Bora za Shayiri zinazozalishwa na Wakala wa Mbegu Bora nchini ASA badala ya kutegemea tu Mbegu wanazopata kutoka katika Makampuni ambayo ndiyo wanunuzi wa zao hilo.

Akiwa na ujumbe wake wa Viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Kilimo, Mkoa wa Arusha pamoja na Wadau mbalimbali wa Kilimo katika Shamba hili la ASA waliweza kutembelea katika eneo ambalo Ngano na Shayiri hulimwa ambapo mbali na shamba hili la Ngaramtoni mkoani Arusha Wakala pia hulima mazao haya katika mashamba mengine ya Dabaga mkoani Iringa na Shamba la Mbozi mkoani Songwe.

Naibu Waziri amezitaka pande tatu ambazo ni Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania – TARI, Wakala wa Mbegu Bora za Kilimo nchini -ASA na Wanunuzi wa Mazao haya ya Ngano na Shayiri kukaa pamoja na kuwezesha Wakulima wa Mazao haya kunufaika na fursa hii kwani upatikanaji wa Mbegu Bora  kupitia Wakala upo na soko lipo pia.

  • Pichani Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu bora za Kilimo nchini ASA akifafanua jambo wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mhe. Hussein Bashe alipotembelea Shamba la Wakala, Ngaramtoni mkoani Arusha