Skip to main content
Habari na Matukio

NFRA WATAKIWA KUONGEZA WIGO WA MAPATO-KUSAYA

Shinyanga

Wizara ya Kilimo imeiagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kubuni njia muafaka ya kuongeza mapato kwa  kuhifadhi nafaka zaidi na kufanya biashara ya mazao ya kilimo.

Agizo hilo limetolewa leo  (28.04.2020) mjini Shinyanga na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli zinazofanywa na wakala kanda ya Shinyanga.

“Kuanzia sasa nataka kuona NFRA inafanya kazi kwa kujitegemea zaidi bila kutegemea fedha za serikali kwa kubuni mikakati ya kutumia uwepo wa vihenge vya kisasa na ghala vinavyojengwa na serikali hapa Shinyanga” alisema Kusaya

Alibainisha kuwa serikali inatekeleza mradi mkubwa wa shilingi Bilioni 15.24 wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi kwa kujenga vihenge (silos) sita zenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na ghala moja kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 za nafaka katika eneo la Ibadakuli mkoani Shinyanga.

Alieleza kuwa mradi huo ni wa mafanikio kwani utawezesha uhifadhi wa mazao toka kwa wakulima kuongezeka toka tani 14,500 za sasa hadi tani 44,500 kwa mwaka utakapokamilika mwezi Juni mwaka huu.

“Tafuteni mbinu itakayoifanya NFRA mhifadhi nafaka nyingi zaidi kama mahindi,choroko,maharage ,mpunga na ziada muweze kuuza na kupata fedha za kujiendesha kibiashara ikiwemo kutumia fursa ya mahitaji makubwa ya nafaka hususan chakula kwenye nchi za jirani na Tanzania” alisitiza Kusaya.

Katika hatua nyingine Kaimu Meneja wa Kanda ya Shinyanga Meriana Yateri ameishukuru serikali kwa uamuzi wake wa kujenga vihenge vya kisasa na ghala kwani vitasaidia kuongeza uwezo wa kanda na nchi kuhifadhi mazao mengi yatakayotumika wakati wa dharura na majanga.

Mwisho.