Skip to main content
Habari na Matukio

Serikali yaongeza uzalishaji katika mazao makuu ya chakula nchini na kujitosheleza kwa chakula 100%

Serikali imeongeza uzalishaji katika mazao makuu ya chakula hususan mahindi, mchele, mtama, uwele, na mikunde jambo linalopelekea kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 100.

Aidha, Uzalishaji mwingine umeongezeka kwenye mazao ya jamii ya mizizi kama muhogo, ndizi, viazi vitamu na mviringo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Wiliam Tate Ole Nasha (Mb) wakati akizungumza na Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wadau wa kilimo Mifugo na Uvuvi na wananchi kwa ujumla wakati wa uzinduzi wa sikukuu ya wakulima – nane nane, Maonesho yenye kauli mbiu ya “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati” yanayofanyika Kitaifa kwenye uwanja wa maonesho ya kilimo wa Ngongo Mkoani Lindi.

Amesema kuwa Katika mwaka 2015/2016 Sekta ya Kilimo ilichangia asilimia 29.1 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 29.0 mwaka 2014/2015. Mchango mkubwa katika Pato la Taifa ulitokana na Sekta ya Kilimo, ikifuatiwa na Sekta nyingine za kiuchumi.

Mchango huo mkubwa ni Kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanashiriki katika shughuli za kilimo, hivyo kilimo kinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato na kupunguza umaskini.

Mhe. Nasha amesema kuwa uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi umeimarisha zaidi usalama wa chakula na lishe nchini, ambapo katika mwaka 2015/2016 uzalishaji wa chakula ulikuwa ni tani milioni 16.2 ikiwa ni ongezeko la tani milioni 0.7 (sawa na 4.5%)  ikilinganishwa na tani milioni 15.5 mwaka 2014/2015.

Uzalishaji wa mazao ya nafaka umeongezeka kutoka tani milioni 8.9 mwaka 2014/ 2015 hadi tani milioni 9.5 mwaka 2015/ 2016 ikiwa ni ongezeko la tani milioni 0.6 (sawa na 6.7%).  Uzalishaji wa mahindi umeongezeka kutoka tani milioni 5.9 mwaka 2014/2015 hadi tani milioni 6.1 mwaka 2015/2016 sawa na ongezeko la tani milioni 0.2 (sawa na 3.4%). Uzalishaji wa mchele uliongezeka kutoka tani milioni 1.9 mwaka 2014/ 2015 hadi tani milioni 2.2 mwaka 2016 sawa na ongezeko la tani milioni 0.3 (sawa na 15.8%).

Vilevile, uzalishaji wa mazao ya chakula yasiyo nafaka umeongezeka hadi kufikia tani milioni 6.7 ikilinganishwa na tani milioni 6.6 kwa mwaka 2014/ 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la tani milioni 0.1 (sawa na 1.5%).

Kwa ujumla uzalishaji wa mazao ya chakula ukilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.2 ya chakula na matumizi mengineyo katika mwaka 2016/2017 unaonesha kuwepo kwa ziada ya tani milioni 3.0 za chakula. Kutokana na hali hiyo Taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 123 ambayo ni ongezeko la asilimia 3 ikilinganishwa na asilimia 120 ya mwaka 2015.

Katika mwaka 2016/2017 idadi ya mifugo nchini imefikia ng’ombe milioni 28.44, mbuzi milioni 16.67 na kondoo milioni 5.01. Pia, wapo kuku wa asili milioni 37.43, kuku wa kisasa milioni 34.5, nguruwe milioni 1.85 na punda wapatao  572,357. jumla ya mitamba 634 ilizalishwa kutoka mashamba ya Serikali na Kampuni ya Ranchi za Taifa - NARCO ikilinganishwa na mitamba 646 iliyozalishwa mwaka 2015/2016. Aidha, jumla ya mitamba 10,820 ilizalishwa na Sekta binafsi na kusambazwa kwa wafugaji wadogo nchini ikilinganishwa na mitamba 10,803 iliyozalishwa mwaka 2015/2016.

Mhe Nasha alisema kuwa Vituo vya Kanda vimeendelea kuimarishwa kwa kupatiwa vitendeakazi,  ukarabati wa miundombinu na mitambo ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya uhimilishaji wakati wote.

Jumla ya dozi 100,000 za mbegu bora za mifugo zilizalishwa ikilinganishwa na dozi 80,000 mwaka 2015/2016. Pia, ng’ombe waliohimilishwa wameongezeka kutoka 221,390 mwaka  2015/2016 hadi ng’ombe 457,557 mwaka 2016/2017.