Skip to main content
Habari na Matukio

SERIKALI IMEAMUA KUHESHIMU NA KUWEKA KIPAUMBELE SEKTA YA KILIMO

NAIBU Waziri wa Kilimo,Husein Bashe amesema Serikali imeamua kuheshimu na kutoa kipaumbele mazao ya kilimo kama sekta zingine zinavyothaminiwa kwa kujenga miundo mbinu rafiki kwa mkulima hususani pembejeo bora.

Kauli hiyo ameitoa wakati alipokuwa kwenye mkutano wa kitaifa wa wakulima wadogo Tanzania uliofanyika jijini Dodoma kujadili changamoto wanazokumbana nazo ulioandaliwa na Shirika la ANSAF.

Waziri Bashe amesema kuwa sekta ya kilimo imekuwa msaada katika kuinua uchumi wa nchi kutokana na kaya ,jamii kwa ujumla kutumia malighafi nyingi zinazotokana na kilimo mbali na changamoto zinazowakabili wakulima .

Amebainisha tarari serikali imeweka mikakati ya kuboresha miundo mbinu kwa wakulima wadogo katika suala zima la kuongeza maafisa ugani vijijini huku wakishirikana na maafsa watendaji kutembelea wakulima,pembejeo zilizo bora na bei rahisi,upatikanaji wa mbegu nzuri,sheria ya kulinda wakulima,kuwapatia Bima ya mazao ,pamoja na kuongea na taasisi za kifedha kupata mikopo yenye riba nafuu jambo ambalo litasaidia kuleta maendeleo.

"Kama Wizara itaendelea kutangaza  na kuhamasisha wakulima wadogo kuboresha miundo mbinu ili kuwe na kilimo chenye tija  kwani wamekuwa wachangiaji wazuri uchumi wa nchi na jamii imategemea chakula kutoka kwa wakulima wadogo"alisema Waziri Bashe.

Hata hivyo amepiga marufuku kwa viongozi wa Ushirika ambao sio wakulima kuongoza wakulima kutokana na malalamiko yanayotolewa ambapo wao kazi kubwa ni kujinufaisha badala ya kuwasaidia wakulima hao.

"Kuanzia leo kiongozi ambaye sio mkulima hapaswi kuongoza wakulima haiwezekani wewe sio dhehebu ya kiislamu halafu eti uwaongoze waislamu"amesema.

Mbali na hayo amesema wizara imeanzisha Dawati la masoko ambalo litashughulikia wakulima ambao ufanyiwa ukiritimba na TBS huku akisema kutakuwa na huduma bure ya mawasiliano ambayo itawala fursa wakulima kupiga simu kueleza changamoto zao na kutatuliwa hapo hapo.

Nae mwenyekiti kamati ya Bunge kilimo,mifugo na maji Mahamoud Mgimwa amesema wabunge wako tayari kuendelea kuwatetea wakulima ili serikali iweze kutatua changamoto zao lengo ni kufikia asilimia kumi .

Kwa upande wake  Mwenyekiti jukwaa la wakulima wadogo wanawake ,Janeth Nyamayahasi amesema wanakumbana na changamoto ya upungufu wa maafisa ugani vijijini kwenye sekta ya mifugo,kilimo na uvuvi na kwamba baadhi ya wataalamu hao hawatoi ushirikiano na mara utoa ushauri mbovu unaopelekea mazao yao kuharibika.