Skip to main content
Habari na Matukio

Serikali Kushirikiana na FAO Kupambana na Sumukuvu na Uhifadhi Bora wa Mazao baada ya Kuvuna

Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi na pamoja na Shirika la Chakula Duniani (FAO) leo wametia sahini juu miongozo ya mashirikiano baina yao lengo likiwa ni kupambana na tatizo la sumukuvu katika baadhi ya maeneo hapa nchini pamoja na uboreshaji wa uhifadhi wa chakula baada ya kuvunwa.

Akiongea na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo hapa Dar es Salaam, Mwakilishi wa FAO nchini Bwana Fred Kafeero amesema makubaliano hayo yatahusisha miradi mitatu ambayo ni kupambana na sumukuvu, kusaidia vikundi vya wakina mama Mkoani Kagera waliokumbwa na maafa ya tetemeko la ardhi na kusaidia namna bora ya uhifadhi wa mazo baada ya mavuno.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo Na Uvuvi (KILIMO) Eng. Mathew pamoja na Mwakilishi  Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Bwana Fred Kafeero

(Image:Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo Na Uvuvi (KILIMO) Eng. Mathew pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Bwana Fred Kafeero)

Bwana Kafeero aliongeza kwamba miradi hiyo inachukua kipindi cha miaka minne na ina thamani ya dola za kimarekani 17,641,000 kwa ujumla.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Eng.Mathew Mtigumwe amelishukuru shirika la chakula duniani kwa kukubali kushirikiana na serikali katika kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo kwa sasa.

Eng. Mtigumwe amesisitiza kuwa serikali kwa kushirikiana na FAO watatumia sehemu ya mradi huo kuelimisha wananchi hasa wa Kanda ya kati ili kuepukana na matatizo yanayoweza kusababishwa na aina hiyo ya sumu.