Skip to main content
Habari na Matukio

SOKO LA MAZAO YA KILIMO KUJENGWA LONGIDO

Dodoma                                                                               

 

Wizara ya Kilimo inatarajia kuanzisha ushirikiano na Wilaya ya Longido kwa ajili ya kufanya uwekezaji na uendelezaji wa eneo la kilimo lenye ukubwa wa ekari 50 katika mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Namanga.

 

Kauli hii imetolewa leo (11.01.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe alipofanya kikao na Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe. Frank Mwaisombe  ofisini kwake jijini Dodoma.

 

“Ni wajibu wa wizara ya kilimo kuhakikisha mazao ya kilimo yanapata soko la uhakika na kuongezwa thamani ili kuwanufaisha wakulima,hivyo uwepo wa soko la mazao mpakani Namanga utasaidia serikali kuongeza mapato” alisema Mhandisi Mtigumwe.

 

Katibu Mkuu huyo alisema wizara kwa kuanzia itatuma wataalam kwenda Longido wiki ijayo ikiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Masoko kuweka mpango mahsusi wa kuwezesha serikali na wawekezaji kutumia eneo hilo la kilimo

 

Aliongeza kusema kuwa wizara ya Kilimo kupita ushirikiano hu inataka kuona eneo hili la mpakani linakuwa kituo kikuu cha uwekezaji kwenye kilimo,kwani ni jukuma la wizara kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima kupata masoko ya mazao yao.

 

“ Wataalam wakae chini baada ya kutembelea Longido na kuweka mpango wa uanzishwaji soko na maghala kwa ajili ya mazao ya kilimo mapema” alisisitiza Katibu Mkuu huyo.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Longido Frank Mwaisombe aliyeongozana na wataalam wa kilimo na ardhi wa halmashauri alisema ushirikiano na wizara ya kilimo unahitajika ili kujenga soko,maghala na viwanda vitakavyoongeza thamani ya mazao kabla ya kuuzwa.

 

Mwaisombe alisema uwepo wa soko na viwanda vya mazao ya kilimo mpakani Longido kutawanufaisha wakulima na wafanyabiashara kuuza mazao yao kwa bei nzuri na nchi kupata pato zaidi.

 

“Tunayo fursa nzuri ya kushirikiana na wizara hii kuimarisha masoko ya mazao ya kilimo kabla hayajauzwa  nje ya nchi,hivyo kuboresha maisha ya wakulima kama anavyoelekeza Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe Magufuli” alisema Mkuu wa Wilaya ya Longido

 

Wilaya ya Longido iliyoanzishwa mwaka 2016 ipo mpakani na nchi ya Kenya ambapo kwa mwaka zaidi ya shilingi Bilioni 54 zinakusanywa kama mapato toka ushuru hususan mazao ya kilimo.

 

Aliongeza kusema Halmashauri ya Longido hukusanya kati ya shilingi milioni 300 kwa mwezi toka ushuru na tozo mbalimbali mpakani hapo,hivyo uwepo wa soko la kilimo utasaidia kuongeza wigo wa mapato toka mazao ya kilimo yanayopitishwa kwa wingi mpakani kwenda Kenya na Somalia.

 

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya hiyo aliyataja mazao ya kilimo yanayongoza kupita mpaka wa Namanga kuwa ni mahindi,vitunguu,nyanya na mazao ya mbogamboga na matunda mengi yakiwa hayajaongezwa thamani.

 

Kikao hiki kimefuatia ziara aliyoifanya Katibu Mkuu Mhandisi Mtigumwe kutembelea halmashauri ya Longido mwanzoni mwa mwaka huu 2020 kwa mwaliko wa Mkuu wa wilaya hiyo Frank Mwaisombe ili kuona namna wizara itakavyosaidia kutumia fursa ya mpaka kukuza masoko ya mazao ya kilimo kwa manufaa ya wakulima nchini.

 

Mwisho.

 

Imeandaliwa na ;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Kilimo

DODOMA

11.01.2020