Skip to main content
Habari na Matukio

TANZANIA NI NCHI SALAMA,WAWEKEZAJI JENGENI VIWANDA- MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuja Tanzania na kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ikiwemo zao la mkonge.

Ametoa wito huo leo (21.01.2021) wakati akikagua shamba la mkonge la mwekezaji Kigombe Estate la Muheza wilayani Tanga ambapo amempongeza mwekezaji huyo kwa kazi nzuri ya kilimo cha kisasa cha mkonge na kumtaka afungue kiwanda cha kuchakata bidhaa zitokanazo na mkonge.

Waziri Mkuu Majaliwa aliwaambia wakazi wa Muheza kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha nchi inaendelea kuwa yenye amani na usalama ili wawekezaji na wananchi wafanye shughuli zao za kujiletea kipato ikiwemo kilimo.

“ Tanzania ni nchi iliyo salama,hivyo tunawaalika wawekezaji kuja kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ikiwemo zao la mkonge hapa mkoani Tanga” alisisitiza Waziri Mkuu

Akizungumza na wakulima na wafanyakazi wa shamba hilo la mkonge Majaliwa alisema ziara yake mkoani Tanga ni mahususi kwa ajili ya kuhamasisha kilimo cha mkonge kutokana na faida zake kiuchumi kwa kuwa hapo zamani wakulima wengi walianza kukata tamaa.

Akitaja faida za kiuchumi za zao la mkonge ,Waziri Mkuu Majaliwa alisema zao hilo hutoa nyuzi zinazotumika kuzalisha vifungashio ikiwemo magunia ambayo ni muhimu kwa utunzaji mazao.

Faida zingine zitokanazo na zao la mkonge ni pamoja na uzalishaji dawa za kuua wadudu, sukari, mbolea kwa ajili ya shambani na pombe (vileo) hivyo wawekezaji wa viwanda vya kuchakata zao la mkonge wanaalikwa kuja Tanzania.

Majaliwa aliongeza kusema serikali inatilia mkazo ujenzi wa viwanda ili kukuza ajira kwa watanzania,kuongeza mapato yatokanayo na tozo na kodi na upatikanaji wa elimu juu ya kilimo cha mkonge kwa wananchi wengi.

“Tumieni maeneo haya ya Handeni, Pangani ,Muheza na Tanga yaliyowazi kulima mkonge. Mkonge si zao la matajili pekee,hata wananchi mmoja mmoja anaweza kulima na kupata kipato cha uhakika huku mkiendelea kulima mazao ya chakula” alisisitiza Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu huyo ametoa agizo kwa wawekezaji wote waliochukua mashamba ya makonge toka miaka ya 1970s lakini sasa hawalimi, kuwa waanze mara moja kuyafufua na kupanda mkonge vinginevyo serikali itawanyanganya na kuyagawa kwa wakulima wadogo wadogo.

Ili kuhakikisha wakulima wengi nchini wanalima zao la mkonge Waziri Mkuu ameagiza Bodi ya Mkonge nchini kuwatembelea wakulima mashambani na kutoa elimu na hamasa pia huduma za ugani.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigella amewapongeza wawekezaji wa shamba la mkonge Kigombe Estate kwa uzalishaji mzuri ikiwemo kuajili wananchi zaidi ya mia tatu shambani hapo.

Shigella ameongeza kusema wataendelea kutoa ushirikiano na mazingira wezeshi kwa wawekezaji wengi zaidi watakaokwenda Tanga kuanzisha mashamba ya mkonge na mazao mengine ili wakuze uchumi wa nchi na kusaidia wananchi kupata kipato.

Naye Mkurugenzi wa Shamba la Mkonge Kigombe Cuthbert  Neil alipongeza serikali kwa ushirikiano inaotoa kuwezesha kampuni hiyo kufanya kazi zake  kwa amani na utulivu.

Neil aliongeza kusema shamba la Kigombe limepokea maelekezo ya serikali ya kuzalisha miche bora ya mkonge na kugawa kwa wakulima wanaozunguka pia kutoa elimu kwa wakulima.

Mwisho

Imeandaliwa na

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

MUHEZA

21.01.2021