Skip to main content
Habari na Matukio

TIJA KWENYE KILIMO NDIO KIPAUMBELE- PROF. MKENDA

TIJA KWENYE KILIMO NDIO KIPAUMBELE - PROF. MKENDA

Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda amesema kipaumbele chake ni kuona wakulima wanaongeza tija kwenye uzalishaji wa mazo nchini kwa kutumia eneo dogo kuzalisha mazo mengi zaidi na kukuza uchumi wa kaya na taifa.

Waziri wa Kilimo amesema hayo hivi karibuni wakati akikakabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa Kilimo  Japhet Hasunga hafla iliyofanyika makao makuu ya wizara ya Kilimo Mtumba jijini Dodoma .

Hafla ya makabidhiano imefanyika kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kumteua Prof. Mkenda kuwa Waziri wa Kilimo katika awamu hii ya pili ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano.

“Sekta ya kilimo inachangia asilimia 28 ya pato la taifa lakini sekta ndogo ya mazao inachangia asilimia 18 ambapo tija ni ndogo. Tija kwenye kilimo ni ndogo sana wakati theluthi mbili ya watanzania inategemea kilimo kwenye maisha ambapo asilimia karibu 70 imejiali huko”. alisema Prof. Mkenda.

Katika salamu zake Mhe. Hasunga amesema anamshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini na kumteua kuongoza wizara ya kilimo kwa miaka miwili ya awamu yake ya kwanza na kuwa alifanya kazi kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula.

“Nimefanya kazi miaka miwili kama Waziri wa Kilimo, nafurahi katika kipindi chote cha kwanza cha awamu ya tano nchi imeweza kujitoshelevu kwa chakula” alisema Hasunga.

Hasunga alisema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiwango kikubwa na msukumo wa uongozi wa Rais Magufuli pamoja na wakulima wa Tanzania waliotikia kauli mbiu ya kufanya kazi kwa bidii.

Waziri huyo mstaafu na mbunge wa Jimbo la Vwawa mkoa wa Songwe aliongeza kusema ataendelea kuwa mwaminifu na kuiomba wizara ya kilimo kutilia mkazo suala la upatikanaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora, viuatilifu, mbolea na zana bora ili kilimo kikue na kuchangia zaidi kwenye pato la taifa.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda alisema atahakikisha sekta ya kilimo inaongeza kuchangia ukuaji wa uchumi toka wa sasa wa asilimia 28 hadi zaidi huku sekta ya kilimo mazao ikitoa mchango mkubwa kwenye upatikanaji wa maligahfi za viwanda.

Katika kuhakikisha sekta ya kilimo inatoa mchango mkubwa kwenye kwenye ukuaji wa uchumi nchi, Prof .Mkenda maetaja mambo makuu manne ambayo ni diara kwake wakati akiongoza Wizara ya Kilimo.

Kwanza kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa kutumia eneo dogo kuvuna mazao mengi hivyo taasisi ya utafiti (TARI) na wakala wa mbegu (ASA) wana jukumu la kuongoza kwenye utafiti wa mbegu bora nyingi ili wakulima wazalisha zaidi.

Pili, kusimamia na kuelimisha mbinu bora za uzalishaji (Good agricultural practices) ambapo amelenga kufanya umwagiliaji kwa njia ya matone ukue na kuchangia kwenye uhakika wa chakula ikiwemo upatikanaji wa viutalifu na huduma za ugani kwa karibu zaidi .

Mkakati wa tatu Prof. Mkenda ameutaja kuwa ni upatikanji wa masoko ya uhakika wa mazao ya wakulima kwa kusimamia masoko ya kimkakati na kufanya wakulima wanufaike na jasho lao kwa faida huku nchi ikiwa na uhakika wa chakula na malighafi.

Mwisho Prof Mkenda amesema katika uongozi wake ndani ya Wizara ya Kilimo atahakikisha upatikanaji wa mitaji na uwekezaji kwenye kilimo unaluwa rahisi na wenye kunufaisha makundi ya vijana na wawekezaji ambapo atatoa mkazo kwenye upatikanaji wa mitaji kupitia miko yenye riba nafuu toka taasisi za fedha nchini na zile za nje ya nchi.

Ka upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alisema kuwa Wizara inazo changamoto ikiwemo kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa upatikanji wa sukari ambapo wa sasa upungufu ni zaidi ya tani 60,000 kila mwaka na upande wa upatikanaji mafuta ya kula upungufu ni zaidi la tani 365, 000 .

Kusaya alitoa wito kwa viongozi wakuu wa wizara wapya kushirikiana na watumishi ili kuhakikisha lengo la serikali ya awamu ya tano la kufikia hekta milioni moja na laki mbili zinafikiwa na kufanya sekta hiyo ichangie zaidi kwenye ukuaji wa uchumi kwani Tanzania ina eneo la hekta milioni 29 zinazofaa kilimo cha umwagiliaji kati ya hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo.