Skip to main content
Habari na Matukio

TUMEDHIBITI KWA MAFANIKIO VISUMBUFU VYA MAZAO NA TUTAENDELEA KUVIDHIBITI - WAZIRI MKENDA

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 13 Mei, 2021 amewatoa hofu Watanzania kuhusu uwepo wa wadudu na ndege waharibifu wa mazao na mimea nchini wakiwemo nzige wa jangwani, nzige wekundu, ndege aina ya kwelea kwelea na viwavijeshi vamizi na kusema Serikali imejipanga kuwadhibiti kabla hawajaleta madhara.

Waziri Mkenda amesema Serikali imekuwa ikidhibiti kwa mafaniko makubwa na itaendelea kuwadhibiti (Visumbufu) hivyo ili kuhakikisha visumbufu hivyo, havileti madhara kwa Wakulima na Wananchi kwa ujumla.

Waziri Mkenda amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inawahakikishia Wakulima na Wananchi kuwa udhibiti wa visumbufu vya mazao na mimea nchini utapewa kipaumbele ili kuondoa tishio la aina yoyote.

Akitoa tathmini ya udhibiti wa nzige wa jangwani waliovamia mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjarao na Tanga; Waziri Mkenda alisema kuwa kwa nyakati tofauti kati ya tarehe 14 Januari, 2021 na 24 Februari, 2020 mikoa ya Kaskazini ilivamiwa na nzige wa jangwa waliotokea nchi jirani ya Kenya na kuingia katika Wilaya nane (8) za Mwanga, Siha na Moshi (Kilimanjaro), Simanjiro (Manyara); Longido, Monduli na Ngorongoro (Arusha); na Lushoto (Tanga).

Kati ya Wilaya hizo, nzige walikuwa wakihama kutoka kwenye maeneo waliyoingia na kulala maeneo mbalimbali ya Wilaya nne (4) Siha (Kilimanjaro), Simanjiro (Manyara), Longido na Monduli (Arusha) wakitanda kwenye eneo la jumla ya hekta 6,441.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa udhibiti wa nzige wa jangwa ulifanyika kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo ya kuunda timu za Viongozi na Wataalam wa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Viongozi wa mikoa, wilaya, vijiji na Wananchi katika maeneo yaliyoripotiwa; Kufanya uchunguzi wa mahali nzige walipo, kutambua hatua zao za ukuaji na kuwadhibiti.

Njia nyengine ni pamoja na kunyunyuzia kiuatilifu maalum aina ya Fenitrothion kwa kutumia ndege tatu (3) na Helkopta moja (1) kudhibiti makundi makubwa ya nzige wa jangwa na pia kwa kutumia vinyunyuzi (motorized sprayers) kwenye makundi madogo ya nzige pamoja na timu za Wataalam kwa kushirikiana na Wananchi kufanya uchunguzi kwenye maeneo yote ambayo nzige walidhibitiwa ili kubaini endapo waliangua mayai na kudhibiti tunutu waliozaliwa.

“Hadi tarehe 04 Machi, 2021 tumefanikiwa kudhibiti makundi yote ya nzige wa jangwa yaliyoingia nchini na uchunguzi uliendelea kufanyika hadi tarehe 13 Aprili, 2021 haujabaini uwepo wa nzige au tunutu walianguliwa na hakuna uharibifu uliofanywa na nzige hao kwenye mazao ya kilimo”

“Hata hivyo, tunaendelea kufuatilia taarifa za utabiri wa nzige wa jangwa na kuwashirikisha Wananchi ili watoe taarifa endapo kutatokea makundi mapya ya nzige.” Amekaririwa Prof. Mkenda.

Kuhusu nzige wekundu; Waziri Mkenda amesema wapo katika mazalio ya asili ya yaliyopo katika Bonde la Mto Malagarasi (Wilaya ya Kigoma na Kaliua), Mbuga za IKuu/Katavi (Wilaya ya Mpanda), Mbuga za Wembere (Wilaya ya Igunga) na Mbuga za Ziwa Rukwa (Wilaya ya Sumbawanga).

Waziri Mkenda amekiri kuwa kuna mazalio madogo (auxiliary breeding area) yaliyoko kwenye Mbuga ya Bahi (Wilaya ya Bahi) na kuongeza kuwa Wizara ya Kilimo kila mwaka hufanya tathmini ya nzige wekundu kwenye mazalio kwa kuangalia uwepo wao na kuwadhibit endapo wameongezeka.

“Katika msimu wa 2020/2021 Wataalam wa Wizara ya Kilimo kwa kushiikiana na Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu la Kati na Kusini mwa Afrika (International Red Locust Control Organization for Central and Southern Africa – IRLCO-CSA) wamefanya uchunguzi katika maeneo yote ya mazalio ya nzige wekundu kuanzia tarehe 15 Februari, 2021 hadi 29 Aprili, 2021 na kubaini kuwa hakuna tishio la uwepo wa nzige hao.” Amekaririwa Prof. Mkenda.

Kuhusu ndege waharibifu aina ya kwelea kwelea; Waziri Mkenda amesema udhibiti wa kwelea kwelea ulianza tarehe 17 Novemba, 2020 na umeendelea hadi sasa katika Wikaya 22 kwenye mikoa 12 ya Kilimanjaro (Mwanga, Moshi), Arusha (Wilaya ya Meru), Manyara (Simanjiro na Babati), Dodoma (Chamwino, Bahi, Kondoa, Dodoma Jiji), Singida (Singida Vijijini, Itigi, Mkalama), Morogoro (Kilosa na Mvomero), Iringa (Iringa Vijijini), Mbeya (Mbarali), Geita (Geita Vijijini), Mwanza (Sengerema na Kwimba) na Shinyanga (Kishapu na Shinyanga Vijijini) na Pwani (Chalinze).

“Tutaendelea kudhibiti kwelea hao katika maeneo mapya yaliyoripotiwa katika Mkoa Tabora na Simiyu na maeneo ambako tumeshadhibiti ndege hao waharibifu.” Amesisitiza Waziri Mkenda.

Kuhusu Kiwavijeshi vamizi (Fall Armyworm- FAW). Kiwakijeshi vamizi ni kisumbufu kigeni ambacho kimeendelea kuripotiwa katika nchi mbalimbali duniani Tanzania ikiwa nchi moja wapo. Waziri Mkenda amesema Wizara imesambaza mitego ya kunasa nondo wa kiwavijeshi vamizi 289 katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Shinyanga, Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro, Kagera, Katavi, Mara, Simiyu, Geita, Morogoro, Njombe, Iringa, Ruvuma, Tanga, Pwani, Tabora, Lindi, Mtwara, Dodoma, Singida na Kigoma.

Na kuongeza kuwa Wizara imesambaza lita 9,900 za kiuatilifu aina ya Duduma katika wilaya za Hai, Mbogwe, Dodoma Jiji, Iramba, Kilindi, mkoa wa Mara, wilaya ya Simanjiro, Bahi na Morogoro vijijini.