Skip to main content

TUTAPAMBANA NA SOKO LA MUHOGO- MKENDA

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 7/5/2021  amekutana na wadau wa zao la muhogo ili kujadili fursa za masoko zilizopo katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza kipato kwa mkulima.

Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Morena kwa kuhudhuriwa na wataalam kutoka  Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Mambo ya Nje,  Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na TAMISEMI.

Mabalozi walioshiriki kwa njia ya mtandao ni balozi wa China, Uganda, Rwanda  na Burundi. Kwa upande wa taasisi za serikali ni pamoja na TARI,TRA,TBS,Ushirika,SIDO,SUA,TANTRADE. Sekta binafsi ni pamoja na  TPSF, AGRA, ESRF, Serengeti  breweries, CTI  na agroforest. Benki  ni TADB,NMB,CRDB, Equity bank.

Aidha,Prof. Mkenda amepata fursa ya kuzindua mkakati wa Muhogo  na amefurahishwa sana na watafiti wetu ambao wamegundua mbegu  mpya na zenye ubora zaidi. Kauli hii aliitoa baada ya kunukuu hotuba ya Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan alipohutubia Bunge la Tanzania  kwa kuzungumzia  sana kuhusu kilimo,mifugo na uvuvi  hasa utafiti.

Prof. Mkenda amesema kuwa kwa mbegu  ya kawaida  hekta 1 mkulima anapata tani 5 mpaka 8 za muhogo. Kupitia taasisi zetu za utafiti TARI Kibaha imefanya utafiti wa mbegu bora za muhogo  zinazohimili magonjwa mfano batobato na  kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji kwa kupata tani 20,30 hadi 50.

“kilimo bila utafiti hatuwezi kufanya chochote,soko la china la muhogo ni kubwa. Hatutaweza kwenda kwa mkulima anayelima bila tija kupata soko” alisema Mkenda

Hata hivyo ameendelea kusema kuwa serikali ikijikita kwenye kilimo bora  wakulima wataweza kulima kwa tija na kupata masoko ambapo watakuwa wameinua kipato cha  wakulima wadogo wadogo.

Prof. Mkenda ameainisha vipaumbele vya wizara  yake kuwa itawekeza  kwenye utafiti wa wataalam  wa kilimo , kuzalisha mbegu bora zaidi  katika mashamba yote 13 ya ASA na kuitaka taasisi hiyo kulima kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mbegu, kuwekeza kwenye ugani kwa mikoa 3 ya kielelezo ambapo afisa ugani ataweza kumfundisha mkulima kuhusiana na mbegu bora na pia ameahidi kuipatia mikoa hiyo pikipiki 1500 kama kitendea kazi ili  maafisa ugani waweze kuwafikia wakulima kwenye halmashauri zao na kufufua mashamba ya mfano.