Skip to main content
Habari na Matukio

  VYAMA VYA USHIRIKA VYATAKIWA KUSHIRIKI KUFIKISHA MBOLEA KWA WAKULIMA

 

Waziri wa Kilimo Mhe. Husein Bashe ameagiza Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani Ruvuma kuanza kusimamia na kuratibu upatikanaji na usambazaji wa mbolea kwa wanachama wake. 

 

Waziri Bashe ametoa agizo hilo leo tarehe 15 Januari, 2023 wakati wa ziara  ya kikazi Mkoani Ruvuma  alipokuwa akipokea taarifa ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya siku mbili mkoani humo.

 

Mhe. Bashe amesema, Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani humo vimekuwa vinaratibu upatikanaji wa Mbolea na Pembejeo za Korosho, Tumbaku na Kahawa tu kwa wakulima sasa wajipambanue waanze kusambaza mbolea za mazao mengine kama vile Mahindi, Soya na Mbaazi.

 

"Kuanzia mwakani nataka kuona vyama hivi vinaratibu upatikanaji wa Mbolea za mazao mengine ili wakulima waweze kupata mbolea kwa wakati na kwa urahisi kisha kuongeza tija katika uzalishaji" Waziri  Bashe amesisitiza.

 

Aidha,  Waziri Bashe ameziagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika  Tanzania (TCDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kufanya kazi kwa    kushirikiana na kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kupitia  vyama vya ushirika.

 

"Mkifanikiwa kupitishia Mbolea katika Vyama Vikuu sitotaka kusikia kelele kutoka kwa wakulima kuhusu mbolea na wakati Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) mpo na mmesambaa kila Mikoa" Waziri Bashe alisisitiza.

 

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Odo Mwisho amepongeza jitihada za Wizara za kuagiza Mbolea kuwafikia wakulima  kupitia  Vyama Vikuu vya ushirika na kubainisha itasaidia kupunguza usumbufu kwa mkulima mmoja mmoja kufuata Mbolea katika vituo vilivyopo Mijini.

 

Amesema Wakulima wanatoka maeneo ya mbali kufuata Mbolea kwa wakala wa usambazaji hali inayosababisha kutumia muda mwingi katika foleni ya ununuzi wa Mbolea hiyo, hivyo anaamini ikipitia katika Vyama Vikuu kila mkulima atapata mbolea yake kwa muda sahihi na karibu na maeneo ya uzalishaji.

 

Pia, Mheshimiwa Mwisho ameiomba Serikali katika mgao wa ujenzi wa Maghala ishirini mapya Ruvuma ambao unategemea kuanza kujengwa hivi karibuni basi uweze kuzingatie uhitaji wa maeneo na si kurundika maeneo ambayo hayana uhitaji.

 

" Yapo maeneo ambayo Maghala yaliyopo yanajitosheleza nakuomba waziri katika ujenzi wa maghala hayo yajengwe sehemu ambazo kweli zinauhitaji wa maghala hayo ili kuepusha utitiri na mlundikano wa Maghala sehemu moja.