Skip to main content
Habari na Matukio

Waziri Hasunga aanza kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kuiuzia Zimbabwe mazao ya kilimo

Waziri Hasunga aanza kutekeleza agizo la Rais Magufuli la kuiuzia Zimbabwe mazao ya kilimo

 

 

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) Siku ya Ijumaa tarehe 31 Mei ameitisha kikao cha dharura na Wakurugenzi wa Taasisi na Idara mbalimbali za Wizara ya Kilimo lengo ni kuanza kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kuiuzia nchi ya Zimbabwe mahindi na mazao mengine kiasi cha Tani Laki Nane (800,000).

 

Itakumbukwa mapema wiki hii, Rais John Pombe Magufuli alipoitembelea Zimbabwe kwa mwaliko wa Mwenyeji wake Rais Emmerson Mnangagwa. Rais Mnangagwa alimweleza Rais Magufuli kuwa Zimbabwe inakabiliwa na upungufu wa chakula na kuiomba Tanzania iiuzie sehemu ya chakula chake cha ziada ombi ambalo Rais Magufuli alilikubali.

 

Waziri Hasunga amesema ujumbe kutoka Serikali ya Zimbabwe utawasili nchini kuanzia Siku ya Jumanne ya Tarehe 3 Juni na unatarajiwa kuwa nchini mpaka tarehe 7 Juni, 2019.

 

Waziri Hasunga ameongeza kuwa ujumbe huo kutoka Zimbabwe unakuja kwa ajili ya kuangalia na kujiridhisha kuhusu mambo ya msingi kama ubora wa chakula na mambo mengine ya awali.

 

Waziri wa Kilimo amesema kimsingi Serikali zote mbili zimekubaliana kuwasaidia Wananchi kwa njia ya biashara na kuongeza kuwa huu ni mwanzo kwa kufanya biashara endelevu baina ya nchi hizi mbili na kuongeza kwa biashara hiyo, itakuwa endelevu mwaka hadi mwaka.

 

Mhe. Hasunga amesema Zimbabwe imefikiria pia kuanza kununua mazao mengine kama korosho kwa kuwa imeona fursa ya kupata mazao yenye ubora na kwa bei nzuri ipo Tanzania kwamba baadae mazao mengine ya mbegu za mafuta, jamii ya mikunde, mboga na matunda yataanza kununuliwa na Taifa hilo la Kusini mwa Afrika.