Skip to main content
Habari na Matukio

WIZARA YAKAMILISHA MWONGOZO WA KILIMO CHA MPUNGA

Iringa,

Wizara ya Kilimo imekamilisha maandalizi ya miongozo itakayotumiwa na wakulima wa Mkoa wa Iringa kuwezesha kufahamu kanuni na teknolojia bora za uzalishaji na usimamizi wa zao la mpunga baada ya kuvuna.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wadau mjini Iringa jana,Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Marco Ndonde aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo alisema kukamilika kwa miongozo hiyo kutasaidia tija katika kilimo cha mpunga kuongezeka.

Aliongeza kusema Wizara ya Kilimo ina jukumu la kuhakikisha uzalishaji na tija vinaongezeka na pia upotevu unapungua ili kufanya kilimo kuwa cha kibiashara na hatimaye kuwa na usalama wa chakula, lishe na kuongeza kipato.

“Zao la mpunga ni muhimu nchini kwa sababu linachukua nafasi ya pili baada ya mahindi kama zao la chakula na biashara” alisema Ndonde

Alibainisha kuwa takwimu za wizara ya kilimo zinaonesha kwamba uzalishaji wa mpunga kwa sasa ni wastani wa tani nne hadi tano kwa hekta kwenye kilimo cha umwagiliaji ambapo kwenye kilimo kinachotegemea mvua ni wastani wa tani 1.8 hadi 2.

Ndonde aliongeza kusema matokeo ya tafiti zilizofanyika zimeonyesha kuwa uzalishaji unaweza kufikia wastani wa tani 8.0 kwa hekta endapo kanuni na teknolojia bora za kilimo zitazingatiwa.

Katika mkutano huo Wizara ya Kilimo imeipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na Shirika la RUDI kwa utekelezaji wa mradi wa RICE unaotekelezwa katika skimu 12 wenye lengo la  kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la mpunga

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo toka Shirika la Kilimo na Chakula (FAO) nchini Ajuaye Sigalla alisema tayari wamefanikiwa kutoa mafunzo ya moja kwa moja kwa wakulima 3000 wa skimu ya Magozina wengine 9000 wa mkoa wa Iringa kupitia vyombo vya habari.

Ajuaye alisema Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa litaendelea kusaidia juhudi za Serikali katika kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usalama wa Chakula Josephine Amolo alisema Wizara ya Kilimo tayari inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi wa Mazao Baada ya Kuvuna (National Postharvest Management Strategy), kwa lengo la kupunguza upotevu wa mazao nchini.

“Upotevu wa mazao wakati na baada ya kuvuna unakadiriwa kuwa kati ya asilimia 30-40 hali inayotakiwa kudhibitiwa ili wakulima wanufaike na jasholao” alisema Amolo

Miongozo hiyo imeandaliwa ili iweze kutumiwa na wakulima wa Mkoa wa Iringa pamoja na maeneo mbalimbali nchini kuongeza tija kwenye zao la mpunga.

Mwisho.

Imeandaliwa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

IRINGA

07.O2.2020