Skip to main content
Habari na Matukio

BILA MIFUMO THABITI HATUWEZI KUJENGA NA KUIMARISHA USHIRIKA IMARA – KATIBU MKUU KUSAYA

BILA MIFUMO THABITI HATUWEZI KUJENGA NA KUIMARISHA USHIRIKA IMARA – KATIBU MKUU KUSAYA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya amesema majukumu makubwa ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika ambayo ni udhibiti, usimamizi pamoja na uhamasishaji wa Vyama vya Ushirika hayawezi kutekelezwa ipasavyo bila ya kuwa na mifumo thabiti inayojengwa kwa vitendea kazi zikiwemo kompyuta na vyombo vya usafiri.

Katibu Mkuu Kusaya ameyasema hayo leo  tarehe 31 Desemba, 2020 wakati akipokea kompyuta 100 za mezani (Desktop) kutoka kwa Benki ya CRDB; Kompyuta hizo zimetolewa na Benki hiyo kama sehemu ya kuunga mkono utendaji kazi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika hususan eneo la usimamizi na ukaguzi wa mara kwa mara wa Vyama vya Ushirika.

Katibu Mkuu Gerald Kusaya amepokea kompyuta hizo 100 zenye thamani ya shilingi milioni 150 Jijini Dodoma katika ofisi za Tume ya Maendeleo ya Ushirika kutoka kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB nchini Bwana Prosper Nambaya.

Katibu Mkuu Kusaya amesema kompyuta hizo 100 zitaongeza kasi na uwajibikaji ikiwa ni pamoja na kuongeza utoaji wa huduma kwa Wanaushirika kote nchini pamoja na kuongeza ufanisi katika shughuli zote za usimamizi wa Vyama vya Ushirika.

“Kompyuta hizi zinazokabidhiwa leo kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika zitaongeza kasi ya uwajibikaji kwa Watumishi wa Tume katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku katika kushughulikia maombi ya leseni na utoaji wake kwa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kote nchini”.

“Itakumbukwa kuwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha Na.10 ya Mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2019, zinaelekeza kila Mtoa huduma ndogo za fedha nchini zikiwemo SACCOS kutakiwa kuomba leseni kwa mujibu wa sheria hiyo. Hivyo, kutolewa kwa kompyuta hizi kutasaidia Ofisi kusimamia zoezi la utoaji wa leseni (ambazo zimekuwa zikiombwa na kutolewa kwa njia ya mtandao – SACCOS Online Application System).”

“Kuongeza ufanisi na kasi katika utendaji kazi wa shughuli za kila siku kwa Watumishi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, ili kuvisimamia kikamiifu Vyama vya Ushirika kwa njia za mifumo ya kiusimamizi”

“Kuongeza ufanisi katika upatikanaji, utunzaji na utoaji wa taarifa na takwimu mbalimbali za Vyama vya Ushirika kama vile Idadi ya Vyama, Wanachama, Hisa, Mtaji uzungukao, Ukaguzi, Usajili, Kesi na Migogoro, Uwekezaji, Masoko, Madeni n.k.” Amekaririwa Katibu Mkuu Kusaya.

Naye Mrajis wa Ushirika nchini Dkt. Benson Ndiege amesema msaada huo wa kompyuta kutoka kwa Benki ya CRDB utaongeza ufanisi kutokana na Watumishi kadhaa wa Tume hiyo kukabiliwa na upungufu wa vitendea kazi kama kopyuta pamoja na usafiri.

“Tume ya Maendeleo ya Ushirika kazi zetu zilikuwa haziendi vizuri kutoakana na baadhi ya Wataalam kukosa vitendea kazi zikiwemo kopyuta; Kuna Maafisa hawana kompyuta kabisa na hivyo kufanya kazi, wanawasubiri wengine wawe wametoka au wawaombe pale amabapo hazitumiki. Kutolewa wa kompyuta hizi kutaongeza tija kwenye majukumu yetu ya kila siku yakiwemo ukusanyaji wa takwimu, kuratibu mafunzo, kufanya tafiti, kuratibu uhamasishaji na nyingine.”

“Naomba kuwahakikishia Benki ya CRDB kuwa tutaendelea kushirikiana nao katika shughuli za maendeleo ya Wananchi wetu. Hasa pape Benki inayofanya biashara au kuwahudumia Wakulima kwa njia ya kutoa mikopo na ushauri wa kifedha.”

“Tume kupitia Maafisa wake na Vyama vya Ushirika watawasaidia kutoa taarifa za kutosha za Wakulima wanaotaka kukopeshwa na Benki hii.” Amekaririwa Mrajis Mkuu Dkt. Benson Ndiege.

Naye Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa CRDB Bwana Prosper Nabaya akiongea kwa naiba ya Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo amesema Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika na kuongeza kuwa hadi sasa Benki hiyo imewakopesha Wakulima walio kwenye Vyama vya Ushirika zaidi ya bilioni 650.

Bwana Prosper Nambaya ameongeza kuwa CRDB imekuwa ndiyo Benki pekee inayofanya kazi za Wakulima wengi nchi kuliko Benki yoyote.

“Katika mwaka wa fedha wa 2019/20 Benki ya CRDB imetoa jumla ya mikopo ya kilimo ya shilingi bilioni 650 sawa na asilimia 40% ya mikipo yote ya kilimo nchini Tanzania.  Kati ya mikopo hiyo bilioni 495 imeelekezwa kwenye mazao makuu ya kimkakati hivyo kumsaidia zaidi ya AMCOS 472 kupata mikopo kwa ajili ya kuongeza tija kwenye uzalishaji wa kilimo (mikopo ya pembejeo, maghala, ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao, mikopo kwa ajili ya miradi ya ufugaji, uwekezaji kwenye misitu na mazao yake pia uwekezaji kwenye uvuvi.” Amekaririwa Bwana Nambaya.

Bwana Nambaya amesema Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika kufufua Ushirika kwa kuongeza mitaji ili kuhuisha na kuujenga Ushirika imara (TACOBA & KCBL).

“Benki ya CRDB inatoa mchango mkubwa kwa wana ushirika kupitia mafunzo na misaada ya vifaa muhimu vya kufanyia kazi kama vile kompyuta.”

“Tunatoa wito wa kuvikaribisha Vyama vyote vya Ushirika nchini kujiunga na Benki ya CRDB ili viweze kujikwamua kiuchumi na kupata mazingira wezeshi kwenye sekta zote za kiuchumi.” Amekaririwa Mkurugenzi Nambaya.