Skip to main content
Habari na Matukio

BODI ZA MAZAO YA KILIMO WEKEZENI KATIKA UTAFITI-WAZIRI HASUNGA

Na Revocatus Kassimba,

Wizara ya Kilimo-Dodoma Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameagiza wakurugenzi wakuu wa bodi za mazao chini ya wizara ya kilimo kutenga fedha kwa ajili ya kufanya utafiti ili kuongeza tija ya uzalishaji.

Waziri Hasunga ametoa maelekezo hayo tarehe 24 Januari 2020 jijini Dodoma ikiwa ni siku ya pili ya kikao kazi cha Menejimenti ya Wizara, bodi za mazao na taasisi kinacho tathamini utendaji kazi wa nusu mwaka kufikia Disemba 2019.

“Bila kuwekeza fedha za kutosha kwenye utafiti kilimo kitaendelea kukua kwa kasi ndogo, hivyo nawaagiza watendaji wakuu wa bodi kuweka bajeti ya utafiti mwaka 2020” alisema Waziri wa Kilimo Katika kikao hicho wajumbe walionesha kutoridhishwa na mwenendo wa hali ya uzalishaji kwenye mazao ya kimkakati ya biashara kama tumbaku, mkonge,kahawa, pareto na chai.

Akitoa taarifa ya hali utendaji kazi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Stanley Mnozya alieleza katika mwaka 2019/20 jumla ya tani 70,087 zilinunuliwa zenye thamani ya shilingi Bilioni 230.3 Mnozya aliongeza kusema licha ya zao la tumbaku kuwa la pili kwa kuingiza mapato zaidi nchini linakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa uhakika wa soko na uwezo kidogo wa wakulima kuzalisha kutokana na mfumo wa kilimo mkataba kutoeleweka vizuri.

“Bodi inaendelea na majaribio ya aina mpya nne za mbegu ya tumbaku ya mvuke toka China ili kuongeza tija kwa mkulima “ alisema Mkurugenzi Mkuu huyo. Kwa upande wa Bodi ya Kahawa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Prof Jamal Adam imeonyesha uzalishaji wa kahawa kufikia Disemba 2019 ulifikia tani 55,979 kati ya lengo la tani 50,000.

Prof Jamal ametaja aina za kahawa zilizouzwa kuwa ni Robusta tani 22,320 Arabika laini (Mild Arabica) 32,057 na Arabika ngumu (Hard Arabica) tani 1,602 na kuingiza mapato yenye thamani ya Dola za kimarekani 87,527,779 mwaka 2019.

Alitaja sababu ya kufikia mafanikio haya kuwa ni bei nzuri katika soko la dunia na kuongezeka kuwa ubora wa kahawa ya Tanzania iliyokusanywa toka vyama vya ushirika. Prof Jamal alitaja changamoto inayoikabili bodi ya kahawa ni uzalishaji mdogo wa miche bora ya kahawa nchini, ambapo mwaka 2019 walizalisha miche milioni 3.6 kati ya lengo la kuzalisha miche milioni 8.

“Tutaendelea kushirikiana watafiti hususani TARI kuwekeza katika utafiti wa miche ili kufikia lengo la Wizara kuongeza wigo wa wakulima kupanda kahawa bora ” alisema Prof Jamal Wakati huo huo Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameagiza watafiti wa madawa na viuatilifi nchini kutumia zao la pareto kuzalisha viuatilifu bora kwa matumizi ya wakulima.

Hasunga alisema hayo kufuatia taarifa iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pareto Lucas Ayo kusema Tanzania inashika nafasi ya kwanza Afrika na ya pili duniani kwa uzalishaji wa pareto

. ‘’Ni wakati sasa wataalamu kutumia pareto kuzalisha madawa na viutilifu bora kwenye viwanda vya ndani ili kukidhi soko la wakulima na kuepusha uwepo wa viuatiflifu visivyo na ubora”alisisitiza Hasunga Taarifa hiyo ya Bodi ya Pareto ilionesha kuwa hadi kufikia Desemba 2019 tani 1,627 kati ya lengo la tani 2,600 za pareto zilizalishwa nchini na kuliingiza taifa mapato ya shilingi Bilioni 4.28 kufikia Disemba 2019.

Akitoa mchango kuhusu umuhimu wa utafiti, Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) Dkt Geofrey Mkamilo alisema “ tupo tayari kushirikiana na bodi zote za mazao kufantya tafiti zitakazokuja na suluhisho la tija ya mazao kuongezeka” hivyo akashauri bodi za mazao kujipanga kifedha .

Takwimu za uzalishaji mazao nchini zinaonesha kupungua kwa uzalishaji na ubora kwenye mazao ya biashara nchini hali inayopelekea nchi kukosa mapato ya kutosha, hivyo kuhitaji utafiti. Waziri wa Kilimo anaendelea na vikao vya Menejimenti kupitia taarifa za utendaji kazi wa Bodi za Mazao na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara yake na kuweka malengo na mikakati ya kuimarisha utendaji kazi kwa mwaka 2020/2021.