Skip to main content
Habari na Matukio

HATUTAVUMILIA WASHAURI ELEKEZI WAZEMBE MRADI WA SUMUKUVU -ENG.MTIGUMWE

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe amewataka washauri elekezi waliosaini mikataba ya kusanifu miundombinu kwa ajili ya utekelezaji mradi wa kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) kuifanya kazi hiyo kwa weledi na ubora.

Ametoa kauli hiyo jana Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kusaini mikataba mitatu na Makampuni yenye thamani ya Shilingi Milioni 868.7 ,randama mbili za mashirikiano na taasisi za TBS na VETA kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kudhibiti Sumukuvu nchini. “Mfanye kazi kwa weledi sana, sasa Wizara ya Kilimo tunazingatia weledi.

Hatutamvumilia mshauri elekezi mzembe ,tutawasimamia kwa karibu na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kwenye miradi hii ya kudhibiti sumukuvu” alisema Mhandisi Mtigumwe.

Kampuni zilizo saini mikataba ni M/S Digital Space kusanifu karantine ya maabara ya utafiti wa magonjwa ya kibaiolojia,Sundy Merchant Ltd kufanya tahthmini ya awali ya mradi wa Sumukuvu na A.V Consult kufanya usanifu na ujenzi wa maghala 14 ya hifadhi ya mahindi na karanga.

Aidha, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesaini randama ya mashirikiano ya kufundisha vijana mafundi mchundo 400 kutengeneza teknolojia ya kuhifadhi mazao wakati Shirika la Viwango (TBS) limeingia makubaliano na Wizara ya Kilimo kusaidia kutoa elimu kwa wajasiliamali na Wafanyabiashara kuzalisha na kuhifadhi mazao kwa kuepuka sumukuvu ili wapate soko la uhakika na salama katika mnyororo wa thamani ya mazao nchini.

Akizungumza wakati wa utiaji saini Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini Dkt.Pancras Bujulu alisema ni fursa nzuri wamepata kufundisha mafundi mchundo kutengeneza vihenge rahisi kwa ajili ya kuhifadhi mazao ya wakulima ili kulinda afya za watu kwa kutumia teknolojia bora “Ni wajibu wetu VETA kutoa mafunzo kwa vijana nchini ili wazalishe vifaa bora (vihenge) kwa ajili ya kuhifadhi nafaka na kujipatia ajira”

Dkt.Bujulu alisema Aliongeza kusema vijana hawa 400 toka wilaya 18 za Tanzania Bara watakuwa chachu ya kusambaza teknolojia hii rahisi na bora ya uhifadhi nafaka nchini. Mratibu wa mradi wa kudhibiti Sumukuvu (Tanzania Iniatives for Preventing Aflatoxin Contamination-TANIPAC) Clepin Josephat alisema mradi huu wa miaka mitano(2019-2023) unatekelezwa nchini kwa lengo la kuhakikisha usalama wa chakula hususan kwenye mazao ya mahindi na karanga hayachafuliwi na fangasi wanaosababisha sumukuvu.

Aliongeza kusema sumukuvu tangu ilipogunduliwa nchini imesababisha madhara kwa wananchi ikiwemo kuongezeka kwa uwezekano wa kansa ya ini,udumavu kwa watoto chini ya miaka 5 na vifo. Katika mwaka 2016 jumla ya watu 19 walikufa na wengine 68 waliugua na kulazwa kutokana na sumukuvu aina ya Aflatoxin kwenye mikoa ya Dodoma na Manyara ambayo imeathirika zaidi. Mwisho! Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Kilimo DODOMA 10.01.2020