Skip to main content
Habari na Matukio

KATIBU MKUU KILIMO ARIDHISHWA NA SKIMU YA UMWAGILIAJI MVUMI KILOSA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji kijiji cha Mvumi wilaya ya Kilosa ambayo imefikia asilimia 94 ya ujenzi na tayari wakulima wameanza kunufaika .

Ametoa kauli hiyo leo tarehe (15 .05.2020) alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya mradi huo uliopo wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro chini ya mradi wa Kuongeza Tija na uzalishaji wa  zao la Mpunga (ERPP)

“  Nimefurahi kuona skimu ya umwagiliaji kijiji cha Mvumi imefikia asilimia 94 ya kazi zilizopangwa katika mkataba.Nimeridhika na kazi ya mkandarasi huyu kwani tayari wakulima wanatumia maji toka kwenye mifereji iliyokamilika kulima mpunga “ alisema Kusaya

 Katibu Mkuu huyo alisema mradi wa umwagiliaji kijiji cha Mvumi umegharimu shilingi Bilioni 1.97 na utanufaisha wakulima wengi wa zao la mpunga katika wilaya ya Kilosa kuongeza uzalishaji na tija.

Akizungumzia kazi zilizofanyika tayari Mhandisi Emanuel Nobert wa kampuni ya Whitecity International Co.Ltd ya Dar es salaam amesema mradi ulihusisha ujenzi wa mitaro ya umwagiliaji yenye urefu wa mita 1,374 na kukarabati mitaro mingine yenye urefu wa mita 2,690.

Aidha Mhandisi Norbert alisema  wamejenga barabara (access road) yenye urefu mita 6,876 ili kurahisisha usafiri wa mazao na wakulima pamoja na ujenzi wa choo,bafu na kisima cha maji kwa ajili ya wakulima shambani  .

Katika hatua nyingine Kusaya alikagua skimu ya umwagiliaji kijiji cha Kigugu wilaya ya Mvomelo  na kusema hajaridhishwa na kazi ya mkandarasi Gopa Construction Ltd kwa gharama shilingi bilioni 1.93 aliyefikisha asilimia 48 tu tangu alipoanza kujenga tangu Juni mwaka jana 2019 .

 “ Sijaridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa skimu hii ya Kigugu.Mkandarasi hujatimiza wajibu wako.Nataka kufikia tarehe 30 Mei  mwaka huu kazi ikamilike” alisisitiza Katibu Mkuu Kusaya

 Katika ziara hiyo ya kushtukiza Kusaya  pia alikagua ghala la kijiji cha Mbogo Komtongo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 88 na kugharimu shilingi milioni 790.87 chini ya kampuni ya M/s Shekemu   na lile la kijiji cha Kigugu asilimia 92 kwa gharama ya shilingi milioni 816.37 chini ya Mkandarasi M/s Ami & Vai Investment.

Ziara hiyo ya kushtukiza inafuatia ziara aliyofanya Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Kilimo tarehe 22 Aprili mwaka huu alipoongoza ujumbe  wa Makatibu wakuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara,Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Ofisi ya Rais Tamisemi kutembelea miradi hiyo.

Miradi hiyo yote inatekelezwa na Wizara ya Kilimo kupitia Mradi wa ERPP kwa lengo la kusaidia wakulima wa zao la mpunga mkoa wa Morogoro kuongeza uwezo wa kuzalisha na kuhifadhi mazao yao.

Mwisho

 

Imetolewa na :

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

Morogoro.

15.05.2020