Skip to main content
Habari na Matukio

KATIBU MKUU KILIMO AWAAGIZA WAKANDARASI WA SKIMU ZA UMWAGILIAJI KUMALIZA MIRADI HARAKA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Musabila Kusaya, leo tarehe 19 Mei, 2020 amewaagiza Wakandarasi wanne kumaliza miradi ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji haraka iwezekanavyo licha ya kutoa sababu rukuki za kuchelewa kumaliza kwa wakati.

Awali akifungua kikao hicho cha dharura alichokiitisha ili kuwapa nafasi Wakandarasi hao waseme kwa nini Wizara isivunje mikataba nao; Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo aliwaeleza waziwazi kusikitishwa kwa namna walivyoshindwa  kumaliza kazi ya ujenzi wa skimu za umwagiliaji maji katika maeneo tofauti ya mkoa wa Morogoro ndani ya muda wa mikataba.

Wakandarasi walioitwa kujieleza Jijini Dodoma ni Kampuni ya Nakuro JV Comfix Engineering Ltd; Inayojenga Skimu ya umwagiliaji ya Njage (Kilombero); Comfix Engineering inayojenga skimu ya umwagiliaji ya Msolwa Ujamaa (Kilombero) Kampuni nyingine ni Gopa Construction (T) Ltd inayojenga skimu ya umwagiliaji ya Kigugu (Mvomelo) na ya mwisho ni Kampuni ya Lukulo Company Ltd; Inayojenga skimu ya umwagiliaji ya Kilangali (Kilosa).

Baada ya majadiliano yaliyochukua masaa kadhaa Wakandarasi wote waliomba kuongezewa kwa vipindi tofauti ili wamalizie miradi hayo ambayo ipo kwenye hatua tofauti; ombi ambalo lilikataliwa na Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa suala la kuongezewa muda lina mchakato wake na kwamba Wakandarasi wote  walitakiwa kumaliza kazi zao kwa wakati na kukabidhi Miradi yote terehe 30 Aprili, 2020 na kuongeza kuwa kuongeza muda ni kukiuka masharti ya mikataba walijoingia na Mteja wao (Serikali).