Skip to main content

KATIBU MKUU KUSAYA ATOA VIFAA VYENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 242 KWA VYUO VYA MAFUNZO YA KILIMO

Katibu Mkuu Wizaa ya Kilimo Gerald Kusaya leo mchana tarehe 30 Machi, 2021 ametoa vifaa vya mafunzo kwa njia ya mtandao (E- Learning) kwa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vya Serikali na Binafsi vyenye thamani ya shilingi milioni 242.

Vifaa hivyo vya mafunzo kwa njia ya mtandao ni pamoja na Projector - 14; CPU - 14, Televisheni za LCD - 14, Camera - 28, Betri za seli kavu - 14, Inverter - 14, UPS - 84, Rooter za Mtandao - 13, Waya za HDMI - 57; Vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 242,066,959.30.

Katibu Mkuu Kusaya amekabidhi vifaa hivyo kwa Wakuu wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo 29 ambapo Vyuo vya Serikali ni 14 na vya Binafsi ni 15 katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Kusaya amesema vifaa hivyo vya mafunzo kwa njia ya TEHAMA vimetolewa kwa Vyuo vya Mafunzo ya kilimo kwa sababu Vyuo hivyo ni kitovu cha kuzalisha Wataalam wa kilimo kwa lengo la kutoa maarifa na ujuzi kwa Wakulima ili wazalishe kwa tija na kujiongezea kipato.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa vifaa hivyo ni vya kisasa na vitachangia katika kurahisisha utoaji wa mafunzo kwa njia ya mtandao.

“Ili kufanikisha kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao, ni muhimu sana kuwa na vifaa vya kisasa na vyenye uwezo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa mtandao na vifaa vinavyowezesha mtandao huo kutumika.” Amekaririwa Katibu Mkuu Kusaya.

Katibu Mkuu Kusaya aliendelea kusema kuwa “vifaa hivi vitaviwezesha Vyuo angalau kupiga hatua katika dhana ya TEHAMA ili kwamba pale ambapo baadhi ya vitabu havipatikani katika maktaba zetu, wanafunzi na wakufunzi waweze kuvipata kirahisi kwa njia ya mtandao. Aidha, ni matarajio yangu kuwa vifaa hivi vitatumika vizuri kwa manufaa ya wanufaika”.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa Vyuo hivyo bado vinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kufundishia vinavyoendana na mabadiliko ya teknolojia ikiwemo njia ya Mtandao (e-learning).

Wakati huo huo Katibu Kusaya amemshukuru Janet Maro Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi  ya Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) kupitia Mradi wa Kuwezesha Utekelezaji wa Mitaala katika Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo vya Kati (Curriculum Implementation Support for Training Institutes-CISTI) ambapo wamekuwa wako bega kwa bega na Wizara katika kuhakikisha mafunzo yanaboreshwa.