Skip to main content
Habari na Matukio

Marufuku Madalali kuwagalaliza wakulima - Mhe.Hasunga

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (Mb) (tarehe 20 Disemba 2019)amepiga marufuku madalali wa mazao ya kilimo ambao wanatumia nafasi hiyo kuwagalaliza wakulima.

Waziri Hasunga amepiga marufuku hiyo wakati akizungumza kwenye mnada wa zao la Kakao uliofanyika kwenye kijiji na kata ya Ikolo iliyopo Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

Amesema kuwa "kumekuwa na wananchi wasiokuwa waaminifu kwa serikali na wakulima wake ambao wanawaibia wakulima maarufu kama Njemke, Butura, na Kangomba hivyo napiga marufuku biashara hiyo na endapo tukiwakamata tutawachukulia hatua za kisheria"

Waziri Hasunga amewaagiza wanunuzi hao wa Kakao na mazao mengine kuhakikisha kuwa wanawalipa wakulima fedha zao mara baada ya kukamilika kwa minada ili waweze kupata fursa ya kuandaa mashamba katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo.

Waziri huyo wa kilimo alisisitiza kuwa zao la Kakao litasalia kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani chini ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika ili wakulima wanufaike na bei nzuri.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga alisema bado vyama vya ushirika vina matatizo ya kukosa uaminifu unaopeleka viongozi kuwaibia wakulima na kwamba wizara itaendelea kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa watendaji na viongozi wa ushirika nchini.

 “Ni wakati sasa ushirika na wadau kuanzisha viwanda vya kuchakata Kakao ikiwa ni sehemu muhimu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhamasisha sekta ya viwanda.” Alisema Hasunga.

Akiwa kijiji cha Ikolo wilaya ya Kyera Waziri Hasunga ameshuhudia mnada wa Kakao ambapo imeuzwa kwa bei ya shilingi 5,042 kwa kilo moja ambayo ni nzuri kwa wakulima.

 Waziri Hasunga amewasihi wakulima kuendelea kulima zao hilo hukuakiahidi kuwa serikali kupitia wizara ya kilimo itaendelea kusimamia kwa weledi kuongeza tija na uzalishajiikiwemo kutafuta soko la uhakika.

MWISHO