Skip to main content
Habari na Matukio

SERIKALI YAJA NA MKAKATI WA KUWAWEZESHA WAKULIMA WA MIWA KUZALISHA SUKARI

Moja kati ya mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ni kuongeza thamani ya mazao kwa lengo la kutanua wigo wa masoko na kumnufaisha mkulima, hivyo Serikali inakwenda kumuwezesha Mkulima
wa miwa kuwa mzalishaji wa sukari, hali itakayopelekea kuongeza upatikanaji wa sukari nchini, faida kwa mkulima na chanzo cha ajira.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde Tarehe 04 Februari, 2023 alipotembelea Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) Jijini Arusha ambao kwa kushirikiana na Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) wanatengeneza mitambo kwa ajili kiwanda kidogo cha kuchakata miwa na kuzalisha sukari.

"Kupitia mitambo hii inayotengenezwa, ambayo nimejulishwa kuwa ifikapo mwezi Juni, 2023 itaanza kufanyiwa majaribio, mkulima wa miwa anakwenda kuwa na uwezo wa kuchakata miwa tani 200 kwa siku  ambayo ni sawa na tani 20 za sukari. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mkazo katika uchakataji na uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo ili yaweze kuongeza ajira, pato la kaya na Taifa kwa ujumla.

Ni kupitia teknolojia hizi ambazo TEMDO na wadau wengine mnazibuni, zitakwenda kusaidia nchi yetu kuondokana na uuzaji wa bidhaa ghafi nje ya nchi na kuingiza bidhaa ambazo zimechakatwa kutoka katika mazao hayo hayo kwa ajili ya matumizi. Teknolojia hizi zitasaidia pia kupunguza matumizi ya  fedha za kigeni kutokana na ununuzi wa bidhaa nje ya nchi.

Kumekuwepo na changamoto ya miwa ya wakulima kuharibika kwa kukosa soko, kutokana na viwanda vikubwa kuzidiwa uwezo wa kuchakata. Hivyo, viwanda hivi vidogo vya wakulima ambavyo vitakuwa na uwezo wa kuajiri wastani wa watu 150 kwa kila kiwanda, vinakwenda kuwa suluhisho kubwa katika kusaidia miwa ya wakulima isiozee shambani.

Natoa  wito kwa Bodi zote za Mazao zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kufanya kazi kwa ukaribu na TEMDO kwa lengo la kuangalia fursa zinazopatikana kwenye mazao hayo na kuona namna ya kuzitumia ili kuleta maendeleo kwa wakulima na nchi yetu kwa ujumla”Alisema Mavunde

Aidha, Mavunde aliwapongeza Wahandisi wa TEMDO kwa kutengeneza mashine za kuchakata alizeti, karanga, mhogo, mkonge, chikichi na zabibu na kuwasihi kuendelea na bunifu zaidi ambazo zitalenga katika utatuzi wa changamoto mbalimbali kwa wakulima wadogo na kuchangia ukuaji wa uchumi.