Skip to main content
Habari na Matukio

Serikali yasambaza vocha milioni 2.9 kwa Wakulima

Msemaji wa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika Bwana Richard Kasuga amesema kiasi cha vocha 2,999,778 za pembejeo zenye thamani ya shilingi bilioni 78 zimesambazwa katika Mikoa 24 ya Tanzania Bara ili zitumike kufidia gharama ya mbolea na mbegu bora katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016.

Bwana Kasuga aliongeza kuwa wakulima zaidi ya 999,926 watanufaika na mpango huo na kuongeza kuwa vocha hizo zitajumuisha kiasi cha mbolea tani 99,993 huku kiasi cha 49,996 zikiwa ni mbolea ya kupandia na tani 49,996 zikiwa ni za kukuzia ambazo zote hizo zitapewa ruzuku ili kufidia sehemu ya gharama ya bei ya soko.

Bwana Kasuga aliongeza kuwa kiwango cha fidia hiyo ni  asilimia 50 ya bei ya soko kwa kila aina ya pembejeo inayopata ruzuku hiyo. Makampuni 23 ya mbolea na 27 ya mbegu bora yanaendelea kutoa huduma ya usambazaji wa pembejeo katika mikoa husika, na mkulima mnufaika atapatiwa pembejeo zinazotosheleza ekari moja ya mahindi na mpunga.

Aidha Bwana Kasuga ameeleza majukumu ya utekelezaji wa ruzuku ya pembejeo za vocha kuwa yamegawanyika katika ngazi sita ambazo ni; Wizara Kilimo Chakula na Ushirika, Kamati ya Taifa ya Uendeshaji wa Utaratibu wa Vocha, Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji.

Majukumu katika ngazi zote hizo ni pamoja na kutoa elimu ya usimamizi wa utekelezaji wa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, kutambua Kaya zinazonufaika, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku kwa kutumia vocha na kuandaa taarifa za utekelezaji  na kuziwasilisha katika ngazi mbalimbali.

Pia amewataka wakulima kutorubuniwa na Mawakala wachache wasio waaminifu na kwamba mafaniko ya Sekta ya kilimo nchini yanamtegemea mkulima ambaye anatumia vizuri pembejeo kuongeza uzalishaji wa mazao husika. Aidha, kufanikisha mapinduzi ya kijani ni muhimu wakulima kutambua kwamba wanapoteuliwa kupewa vocha wanakuwa wamedhaminiwa na Taifa hivyo watumie dhamana waliyopewa kwa maslahi yao na ya Taifa kwa ujumla”. Alimalizia, Bwana Kasuga.