Skip to main content
Habari na Matukio

BASHE KUINUA ZAO LA ZABIBU DODOMA

Serikali  imeunda timu ya watu 12, huku ikiwapa siku 10 kuhakikisha wanafanya utafiti wa zao la Zabibu kama linaleta hasara au faida kwa mkulima  na Serikali kiujumla.

Aidha timu hiyo pia imeagizwa kujua magonjwa yanayoathiri zao hilo na kujua  mkulima akipanda heka moja inamgharimu kiasi gani. Hii itasaidia kupata takwimu sahihi ya gharama anazopata mkulima kwenye uzalishaji kwani kilimo cha zabibu kina gharama kubwa.

Hayo yalisemwa na Naibu  Waziri wa Kilimo  Mhe.Hussein Bashe katika Mkutano wake na wadau wa zao la zabibu walipokuwa wakijadili changamoto mbalimbali zinazoikabili zao hilo.“Zao la zabibu hapa Dodoma linakua kwa kudra za Mwenyezi Mungu, ndio maana nimeamua kuunda, 'technical team' ili iweze kuleta ripoti tutakayoifanyia kazi”.Alikaririwa akisema

Bashe alisema kuwa zao la zabibu ndio uti wa mgongo wa Jiji la Dodoma hivyo Kuna Kila sababu ya kuweka mpango mkakati kwa ajili ya kuinua zao Hilo. Bashe ameunda kamati ya watu 12 itakayoongozwa na  Mkurugenzi msaidizi kutoka ofisi ya Sera na Mipango  kwa upande wa Sera akiwa  Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambapo wote watafanya utafiti kwa muda wa wiki moja na kuwasilisja ripoti.

"Ripoti itakayoletwa na kamati hii,itatusaidia kujua wakulima wa zabibu wako wangapi? Changamoto za Wakulima,wazalishaji na wasindikaji, hivyo itatusaidia katika mikakati yetu"'alisema Bashe.

Aidha Bashe alisema kuwa, mkakati mwingine wa Serikali ni kufufua mabwawa yote yaliyotengenezwa kwa ajili ya umwagiliaji wa zabibu katika Wilaya tatu zinazolima zao hilo ambazo ni Bahi,Chamwino na Dodoma.

Bashe amewataka wadau wa Kilimo Cha zabibu kuunda Vyama  vya Ushirika ili viweze kusaidiwa kwa karibu na Taasisi za Fedha. Naye MKurugenzi wa Doniya Estate ambaye ni msindikaji wa zao la zabibu Catherine Mwambe alisema kuwa suala la Kodi limekuwa kikwazo kikubwa kwa wazalishaji wa mvinyo.

"Yaani kwa siku moja zinakuja Taasisi zaidi ya Tano Kila moja inakuja kuchukua Kodi, sasa tunajikuta hata faida hatupati, maana hela yote inaishia kwenye hizo Kodi" alisema Mwambe.

Aidha Mwambe alisema, gharama za uzalishaji ziko juu, na Soko la zabibu hapa nchini bado,hivyo waniomba Serikali kuingilia Kati,kuweka mazingira rafiki ya biashara ya zabibu.

Mwisho.