Skip to main content
Habari na Matukio

DKT. SAMIA ASHUSHA NEEMA KWA WAKULIMA WA LINDI MTWARA NA PWANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 20 Septemba 2023, amehitimisha ziara yake ya kimkakati ya siku saba (7) katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani. 

Katika ziara hiyo, Mhe. Rais Samia amefanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuzindua miradi, kuweka mawe ya msingi, kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa matukio na Mikutano takribani 33. 

Katika sekta ya kilimo, ziara  hii ya kimkakati imekuwa ya mafanikio makubwa kwa wananchi ikiwemo kupata taarifa sahihi kuhusu mwelekeo wa Serikali katika sekta ya kilimo kupitia utekelezaji wa mikakati, programu na miradi mbalimbali kama vile utoaji wa pembejeo za ruzuku, kufungua masoko mapya, ujenzi na ukarabati wa miradi ya umwagiliaji, ghala za kuhifadhi mazao, ugawaji wa vitendea kazi kwa maafisa ugani na elimu kwa wakulima kwa tasnia za mazao ya kilimo ikiwemo korosho, ufuta, mbaazi, mpunga, sukari, alizeti na mazao ya horticulture.

Mhe. Rais Samia amepokea shuhuda za shukrani kutoka kwa wananchi walinufaika na pembejeo za zaidi ya Shilingi Bilioni 200 katika zao la korosho ikiwa ni mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya Kilimo. 

Kutokana na jitihada za Serikali za kuimarisha mifumo ya masoko, Mheshimiwa Rais alieleza hatua ya Serikali ya Awamu ya sita ya kuingiza zao la Mbaazi na Ufuta katika Mfumo wa Stakabadhi za  Ghala (Warehouse Receipts System) ambayo imeimarisha bei ya Mbaazi kwa wastani wa Shilingi 2,300 kwa kilo; na kwa zao la ufuta kati ya Shilingi 3,800 hadi 4,000 kwa kilo. 

Alieleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya masoko ya korosho na bidhaa zake ili kuwezesha wakulima kupata bei yenye tija zaidi.

Katika kuimarisha ushindani na kumuongezea mapato mkulima, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) alielezea kwa kina mipango ya Serikali ya kujenga Kongani ya Viwanda vya kuongeza thamani Korosho na Ufuta; na tayari Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo eneo la Maranje, Nanyamba Mkoani Mtwara sambamba na kuanzisha kiwanda cha ukubwa wa kati cha kubangua korosho mkoani Lindi