Skip to main content
Habari na Matukio

DKT TIZEBA ASEMA BEI YA KOROSHO IMEIMARIKA KUTOKANA NA MATUMIZI BORA YA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI

Uwepo wa mfumo wa stakabadhi ghalani umekuwa ni mkombozi pekee kwa wakulima wadogo na wa kati kwa kuwawezesha kupata bei nzuri ya mazao yao, ukilinganisha na bei zilizokuwa zinatolewa na wafanyabiashara wanaponunua mazao yakiwa shambani kwa kutumia vipimo ambavyo sio sahihi.


Kabla ya mfumo huo kuanza wakulima walikuwa wakipunjwa bei ya mazao na wafanyabiashara ambapo hata hivyo kumekuwepo na mwamko miongoni mwa wakulima, kupitia vyama vyao vya msingi, wa kutumia mfumo halisi wa stakabadhi ghalani pasipo kuchukua mikopo toka Taasisi za Fedha. Katika msimu wa mwaka 2017/2018 vyama vyote viliweza kukusanya na kuuza mazao bila kukopa benki.

 

Hayo yamebainishwa tarehe 29 Septemba 2018 na Waziri wa Kilimo Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa wadau wa tasnia ya korosho uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki kuu ya Tanzania tawi la Mtwara.

 

Alitaja kuwa ushirika ni dhana ya kuleta maendeleo kwa kushirikiana, Dhana hiyo imefanikiwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita ambapo uanzishwaji wa vyama vingi vya ushirika kwa sasa unatokana na elimu watu wengi waliyoipata kuhusu Ushirika. “Ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka miwili hivi, imani kwa vyama vya ushirika imeongezeka na vyama vingi vinaendelea kuundwa hasa vile vya kuweka na kukopa, yaani SACCOS” Alikaririwa Dkt Tizeba

 

Dkt Tizeba alitoa wito kwa vyama vya ushirika kuendelee kukusanya korosho kwa msimu huu ili soko na bei iendelee kuwa imara pamoja na kuwa na misuko suko mingi ya masoko Duniani. “Aidha ni vyema Wakulima wote wakajiandisha na kuwa Wanachama wa vyama vya Ushirika amabpo watapata faida nyingi ikiwemo kufanya maamuzi kwa pamoja” Alisema Dkt Tizeba

 

Alitaja mafanikio katika zao hilo kuwa ni pamoja na kuimarishwa kwa usimamizi wa zao, uratibu mzuri wa ununuzi na usambazaji wa pembejeo za ruzuku, usimamizi wa karibu unaofanywa na viongozi wa serikali katika ngazi zote, na hamasa mpya ya wakulima kujishughulisha na kilimo cha korosho katika maeneo asilia na maeneo mapya.

 

Dkt Tizeba alisisitiza kuwa hali hiyo ikiendelea kuna uwezekano wa kuzalisha zaidi ya kiwango cha sasa na kuwa na malighafi inayoweza kutumika kwa mwaka mzima kwa kuuza nje na viwanda vya ndani.

 

Katika hatua nyingine aliongeza kuwa pamoja na kuwa na mafanikio makubwa kwenye zao la korosho lakini zipo changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na kuwepo kwa mashamba makubwa ya mikorosho iliyotelekezwa, Uchelewashaji wa malipo kwa Mkulima, Wanunuzi kulalamikia upotevu wa Korosho, ubora hafifu na ubadhilifu, pamoja na Ucheleweshaji wa malipo toka wa Mabenki kwenda vyama na uwepo wasuspence account ambazo zinaathiri malipo kwa Mkulima.

 

Hivyo katika kufanikisha na kuwa na maendeleo katika zao hilo yanatakiwa kufanyika  mabadiliko ambayo yatahitaji ushirikiano wa wadau na hasa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi katika usimamizi ili kuhakikisha Mkulima anapata fedha kwa Wakati.

 

Ameelekeza kuwa katika msimu huu kila Halmashauri ianzishe sehemu maalumu ya Malipo kwa Wakulima (Payment centre) ambapo wataalamu watasaidia vyama hususani toka Vyama Msingi kwenda kwa Wakulima baada ya ukokotoaji wa gharama mbalimbali na kupeleka benki kwa wakati jambo ambalo litasaidia kubaini mapungufu ya kimalipo kwa mabenki na au unaosababishwa na Watendaji wa Vyama.

 

Waziri Tizeba pia ameelekeza kuwa, Mtiririko wa Malipo kwa Mkulima unapaswa kusimamiwa vizuri na kila Halmashauri ya Wilaya iwe na kituo kitakachorahisisha malipo kwa Mkulima mara baada ya fedha kutoka Chama Kikuu cha Ushirika kwenda AMCOS (Payment Clinc Centre), Secretatiati za Mikoa, Halmashauri, Kamati za Ulinza, Bodi ya Korosho,  Mrajis wa Vyama vya Ushirika na mabenki kushirikiana kuhakikisha jambo hilo linatekelezeka ili kumpunguzia Mkulima adha ya Malipo