Skip to main content
Habari na Matukio

HALI YA MILIPUKO YA VISUMBUFU VYA MAZAO NCHINI

TAARIFA YA HALI YA MILIPUKO YA VISUMBUFU VYA MAZAO  NCHINI

 

UTANGULIZI

Taarifa ya hali ya uvamizi wa visumbufu vya Mimea hususan FAW katika msimu wa 2017/2018 imeanza kupokelewa Wizarani kuanzia mwishoni mwa Desemba , 2017 tarehe 19/1/2018. Hadi tarehe 31/01/20018, taarifa zilizopokelewa ni  kutoka Mikoa ya Singida, Lindi, Simiyu, Kagera, Mwanza, Geita, Iringa, Kilimanjaro, Mbeya, Pwani, Tabora, Shinyanga, Tanga na Ruvuma zinaonesha kuwa:

Jumla ya hekta 71,425.9 za mahindi, mtama na mazao mengine (na kwa uchache kwa kahawa na pamba) zimevamiwa na kiwavjijeshi vamizi Fall Armyworm (FAW)  (Spodoptera frugiperda).
Hekta 47,617.6 zimevamiwa na panya (katika mikoa ya Lindi (Lindi Vijiji, Liwale, Ruangwa, Nachingwe, Kilwa); Kagera (Muleba, Missenyi, Ngara); Mbeya (Chunya); Pwani (Chalinze, Kisarawe, Rufiji, Kibiti); Tanga (Kilindi, Handeni DC, Handeni Mji, Muheza DC, Pangani) na Ruvuma (Songea), mikoa ya Morogoro, Songwe na Arusha zilipitia Kituo cha Kudhibiti Panya  cha Morogoro. Aidha, mikoa mingi haijaonesha eneo lililovamiwa).
Hekta 34,034.2 za mazao aina ya nafaka zimevamiwa na viwavijeshi tulivyozoea (Spodoptera exempta).
Kwelea kwelea waharibifu wa nafaka wameripotiwa kuvamia mashamba ya mtama na uwele Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga. Tathmini ya uharibifu inaendelea kufanyika ya kubaini malao yake ili kurahisisha udhibiti/

HATUA ZILIZOCHUKULIWA HADI SASA

Udhibiti wa FAW

Baadhi ya Halmashauri zimeendelea kuwahamasisha wakulima kutumia viuatilifu vilivyoshauriwa kudhibiti kiwavijeshi vamizi lakini kwa maeneo mengi wameshauriwa kutumia viuatilifu vinavyoua viwavi wengine ambavyo vinaweza kuleta matokeo mazuri kuuangamiza viwavi wachanga wa kiwavijeshi vamizi.

 

Hadi sasa Serikali imepokea jumla ya mitego ya nondo wa viwavijeshi vamizi 305 kutoka FAO, Bytrade na Shirika la Nzige Wekundu. Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Halmashauri wanaendelea kusambaza mitego hiyo. Hadi sasa mitego hiyo imesambazwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam (25); Rukwa (24); Songwe (24); Mbeya (24); Shinyanga (06); Arusha (2);Mwanza (04); na Tabora (10). Kazi ya kusambaza mitego iliyobaki inaendelea. Aidha, Mfumo wa unaswaji wa nondo na utabiri wa milipuko utaimarishwa ili kuweza kutoa taarifa za hatari ya kuwepo kwa milipuko kwa wakulima mapema.

 

Savei ya kubainisha ueneaji wa kiwavijeshi vamizi hapa nchini imeshafanyika kwa baadhi ya maeneo katika mikoa ya Morogoro, Rukwa, Mara, Songwe, Mbeya na Tanga.

 

Elimu ya utambuzi na udhibiti wa FAW imeshatolewa kwa Wataalam wa kilimo na viongozi katika baadhi ya Wilaya katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Dar es Salaam na itaendelea kutolewa.

 

Udhibiti wa Kwelea kwelea

Tathmini ya uharibifu uliokwisha kufanywa inaendelea kwa kuzingatia kuwa bado ndege hao wanaendelea na uharibifu.
Halmashauri kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo wamebaini malalo ya ndege hawa katika Kata ya Mwadui, hivyo utaratibu wa kufuatilia ndege ya kunyunyiza viuatilifu vya kuangamiza Kwelea hao ambayo ipo katika matengenezo Jijini Nairobi unaendelea. Pindi itakapokuwa tayari kazi ya kuwadhibiti itaanza mara moja.  Matarajio ni ndege hiyo kuja nchini tarehe 4.2.2018.

 

Udhibiti wa Panya

Wakulima wanaendelea kutumia njia za asili lakini kwa kiwango kikubwa wanasubiri msaada wa viuatilifu kutoka Serikalini.  Shilingi milioni 246 zimeombwa kutoka Kitengo cha Maafa kudhibiti panya.

 

Viuatilifu vinavyoshauriwa Kudhibiti FAW

Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Tropiki (TPRI) imetoa orodha ya viuatilifu vinavyoshauriwa kwa ajili ya kuangamiza kiwavi vamizi. Viuatilifu hivyo ni vile vyenye viambata amilifu (a.i) vinavyoua kwa kugusa (contact) na chenye kupenya mmea na kumuua mdudu akila mmea huo (systemic) 

 

Taarifa zilizowasilishwa zinaonesha kuwepo kwa changamoto zifuatazo:

Bado kuna uelewa mdogo hata kwa wataalamu wa kilimo kubainisha uharibifu unaofanywa na viwavijeshi wa kawaida, Viwavijeshi vamizi (FAW) na bungua wa mahindi. Hivyo,  elimu zaidi juu ya utambuzi wa kiwavijeshi vamizi kwa wataalam na wakulima ni muhimu.

 

Katika baadhi ya mikoa wakulima wanatumia viuatilifu visivyoshauriwa kwa kisumbufu husika. Mfano wakulima wameripitiwa kutumia viuatilifu vya wadudu kutaka kuangamiza panya. Hivyo, elimu zaidi kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu kwa wataalam na wakulima inahitajika.

 

 

Mipango ya Baadaye

Udhibiti wa kiwavijeshi vamizi

                  

Serikali imeshatoa shilingi bilioni tatu (3,000,000,000) kwa Bodi ya Pamba Tanzania ajili ya kudhibiti visumbufu kwenye zao la pamba ambalo kwa mwaka huu uzalishaji unategemea kuwa tani laki sita (milioni 600) kutokana na ziada ya ekari 3,000,000,000zilizolimwa/
Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) limetoa dola za kimarekeni 250,000 sawa na shilingi 550,000,000 kwa ajili ya kudhibiti FAW
Kwa kuwa mtego mmoja wa nondo wa kiwavijeshi vamizi wana una uwezo wa kuvuta nondo katika eneo la Hekta 0.5 hadi 2, Serikali itaendelea kununua mitego zaidi ili kuimarisha mfumo wa utabiri wa milipuko na taarifa za haraka kwa wakulima.
Kufanya savei ya kubaini ueneaji wa kiwavijeshi vamizi hapa nchini.
Kutoa elimu kwa Maafisa Kilimo (DAICO) katika Halmashauri zote nchini kuhusu utambuzi, matumizi sahihi ya viuatilifu na udhibiti sango wa kiwavijeshi vamizi.
Kuendelea kufanya tafiti zaidi na kutangaza viuatilifu vitakavyobainika kufanya vizuri zaidi na vyenye gharama nafuu katika udhibiti wa kiwavijeshi vamizi; na katika kuongeza wigo wa viuatilifu vya kuua visumbufu hivi.
Kuendelea na tafiti za kubaini vimelea au viumbe hai vya kudhibiti kiwavijeshi vamizi kibaiolojia.
Kufuatilia na kukusanya taarifa mpya za tafiti kuhusu udhibiti wa viwavijeshi vamizi.