Skip to main content
Habari na Matukio

Kamati ya Bunge Yatoa ushauri Kwa Wizara

Kamati ya Bunge iliyotembelea Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hivi karibuni wameishauri Serikali kuongeza juhudi katika kusambaza chakula cha msaada kwa waathirika wa njaa katika Wilaya na Halmashauri zilizokumbwa na tatizo hilo.


Wakiongea kwa nyakati tofauti Wajumbe wa Kamati hiyo wamesema kuwa inachukua muda mrefu kwa chakula cha msaada kuwafikia walengwa kwa sababu ya kuwepo kwa kamati nyingi za ugawaji wa chakula hicho hivyo kuzidi kuwapa hali ngumu walengwa.

Aidha Wajumbe wa Kamati hiyo wamesistizia Idara ya Usalama wa Chakula kutoa ushirikiano mkubwa  kwa  Halmashauri wakati wanapofanya tathimni ili kupata Idadi kamili ya waathirika wa njaa na kuepuka taarifa zisizo sahihi.

Naibu Katibu Mkuu wa  Wizara ya Kilimo Chakaula na Ushirika  Bibi Sophia Kaduma aliieleza Kamati ya Bunge ya Kilimo Maji na Mifugo kuwa  changamoto kubwa kwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ni upatikanaji wa magunia ya kuhifadhia nafaka na idadi ndogo ya maghala.

Alibainisha kuwa kiwanda kinachozalisha magunia ya katani hapa nchini hakina uwezo wa kutosha wa kuzalisha, hivyo kushindwa kusambaza magunia katika taasisi za Wizara ya Kilimo hasa ikizingatiwa kuwa Wizara ina uhitaji mkubwa wa magunia ya kuhifadhia kahawa, pamba na mazao mengineyo katika tasisi zake.

Kuhusu uhaba wa chakula Bibi Sophia Kaduma  amesema kuwa tathimini hufanywa  mapema pindi taarifa zinapopatikana kutoka katika vyanzo  husika.

Wilaya ambazo zimepata upungufu wa chakula zimeshafanyiwa kazi na Wilaya nyingine zilizojitokeza na zinazoendelea kujitokeza zinashugulikiwa haraka alisema Naibu Katibu Mkuu.

Upungufu wa Magala ni changamoto nyingine inayoikabili Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirka ambapo, Wizara ina uwezo wa kuhifadhi Tani Laki Mbili na Elifu Arobaini na Moja tu (241,000) katika maghala yote ingawa lengo ni kuwa na uwezo wa kuhifadhi Tani Laki Nne alisema Naibu Katibu Mkuu