Skip to main content
Habari na Matukio

Kanda ya Sumbawanga yanunua shehena ya mahindi kiasi cha tani elfu 20 msimu wa ununuzi wa 2016/17

Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Sumbawanga, Bwana Morgan Mwaipyana amesema kuwa Wakala, Kanda ya Sumbawanga imefanikiwa kununua mahindi kutoka kwa wakulima na kuvuka lengo kwa zaidi ya asilimia 104 katika msimu wa kilimo wa 2016/2017.

Bwana Mwaipyana amesema katika msimu wa ununuzi uliofungwa hivi karibuni, Kanda ya Sumbawanga ilipewa lengo la kununua mahindi kiasi cha tani 20,000 kwa ajili ya kuweka kwenye akiba yake na kwa kulitekeleza jambo hilo, hadi msimu unafungwa, Kanda ilifanikiwa kununua shehena ya mahindi, kiasi cha tani 24,514.80, na kuvuka lengo kwa zaidi ya asilimi 104.

Bwana Mwaipyana aliongeza kuwa kiasi kikubwa cha mahindi kilinunuliwa kutoka katika Mkoa wa Rukwa na kiasi kidogo kilinunuliwa kutoka Mkoa wa Katavi katika Wilaya ya Mpanda.

Bwana Mwaipyana amesema baaada ya Wakala Kanda ya Sumbawanga kuvuka lengo hilo la ununuzi, ilikubaliwa kuwa ongezeko hilo la tani 4,000, lihamishiwe kwa Kanda ya Kipawa na baadae kiasi hicho kiliamishiwa kwenda katika maghala ya Kipawa ambayo, inahudumia Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga, Morogoro, Mtwara na Lindi ambapo katika maeneo hayo ununuzi haukuwa mkubwa.

Akizungumzia changamoto ya ubora na usafi wa mahindi kwenye msimu wa ununuzi wa 2015/2016, Bwana Mwaipyana amesema, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula siku zote, imekuwa ikisisitiza na kusimamia ubora wa bidhaa kabla ya kununua kutoka kwa wakulima na kwamba wakulima wa Mikoa ya Rukwa na Katavi kwa sehemu kubwa wamejitahidi kuielewa dhana hiyo na kuleta mahindi yenye ubora tofauti na miaka ya nyuma.

“Uzoefu wangu kwa hapa Mkoa wa Rukwa na Katavi umenionyesha kuwa kuna mwamko na uelewa juu ya ubora wa mahindi, napenda kutoa wito kwa wakulima, kuendelea kuzingatia maelekezo ya wataalam, na ikumbukwe kuwa ubora wa mazao kama mahindi, unaanzia kwenye hatua za awali kama ya kuandaa mashamba, kuchagua mbegu, kupanda, kuvuna na mpaka wakati wa kuhifadhi” alikaririwa Bwana Mwaipyana.

Bwana Mwaipya aliongeza kuwa “Na kama hatua zote hizo, mkulima akizifuata na kuzitekeleza kikamilifu, wakati wa msimu wa ununuzi unapofunguliwa na Wakala, ni dhahiri kuwa bidhaa atayoileta, itakuwa na ubora unaotakiwa bila ya uchafu na itakidhi vigezo vya Wakala”

“Pili, natoa wito kwa Wadau wote wa Sekta ya Kilimo, kuendelea kuwaelimisha wakulima wetu kuhusu uhifadhi bora wa nafaka baada ya kuvuna (post-harvest management) ili mwisho wa msimu wapate faida inayokusudiwa na sisi tupate nafaka bora lakini pia tupunguze upotevu wa mazao mara baada ya kuvuna.

“Ambapo takwimu za sasa kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), zinaonyesha upotevu wa mazao baada ya kuvuna, umefikia asilimia 40 mpaka 50, hiki ni kiwango kikubwa”. Alikaririwa Bwana Mwaipyana.

Aidha, Bwana Mwaipyana aliongeza kuwa licha ya kuwa na kiasi kikubwa cha mahindi kinachopotea lakini hata yale yanayobaki ubora wake uwa chini kwa kuwa sehemu kubwa yanakuwa machafu na mengine yanakuwa yamevunjika.

Akizungumzia suala hilo la kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara, Bwana Joseph Ogonga amesema, suala la kupunguza upotevu wa mazao mara baada ya kuvuna linaendelea kutafutia ufumbuzi wa kina na kwamba ni juhudi za muda mrefu za Serikali kwa kushirikisha Wadau mbalimbali.

Bwana Ogonga, anasema awali Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) waliandaa andiko la namna ya kuwaelimisha Maafisa Ugani na wakulima namna ya kupunguza upotevu wa mazao na kwamba kwa sasa, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi ipo kwa maandalizi ya mwisho ya kukamilisha mwongozo mwengine kwa ajili ya kuwaelimisha Maafisa Ugani na wakulima nchini kote.

“Serikali inajitahidi na imeanza kulishughulikia suala hilo na napenda tu nitoe wito kwa Wadau wote wa Sekta ya Kilimo, tuungane katika kuhakikisha tunawasaidia wakulima wetu, suala la kupunguza upotevu wa mazao mara baada ya kuvuna ni suala la Wadau wote na si Wizara tu kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika au Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula au FAO. Sekta Binafsi ina mchango mkubwa katika jambo hili” Alikaririwa Bwana Ogonga.

Kaimu Mkurugenzi, Bwana Ogonga aliongeza kuwa kwa sasa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Makao Makuu, ipo kwenye mazungumzo na hatmae kusaini makubaliano ya kushirikiana na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) ambapo mkakati ni kutoa elimu hiyo kwa wakulima katika Wilaya 21 ambazo wakulima wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo.