Skip to main content
Habari na Matukio

Katibu Mkuu aipongeza Benki ya Dunia kwa Kusaidia Mradi wa EAAPP

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bibi Sophia Kaduma hivi karibuni aliwashukuru Wajumbe kutoka Benki ya Dunia kwa namna ambavyo Taasisi hiyo kubwa ya fedha Duniani, ilivyofadhiri na kufanikisha mradi wa EAAPP ambao, awamu ya kwanza itakamilika, 31 Desemba, 2015.

Bibi Kaduma alisema mafanikio, yaliyopatikana baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo, yamepokelewa na wakulima na wadau wa Sekta ya kilimo kwa mikono miwili na kusisitiza kuwa Tanzania inaunga mkono utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo kama fursa hiyo, itapatikana.

Bibi Kaduma alitoa pongezi hizo katika mkutano maalum mbele ya Wajumbe kutoka Benki ya Dunia na Wasimamizi wa mradi huo kutoka Tanzania ambao ni Idara ya Utafiti na Maendeleo, kutoka Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika  na Idara ya Mifugo,  kutoka Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Bwana Abel Lufafa alimuhakikishia Katibu Mkuu kuwa Benki ya Dunia haitasita kuendelea kufadhiri awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba ameomba wadau wa kilimo kusubiri kikao cha kupitisha maamuzi ya kuendelea na ufadhiri huo.

Bwana Lufafa alisema siku zote Benki ya Dunia ipo tayari kusaidia miradi yote yenye lengo la kuwasaidia wakulima, na hasa yenye kuleta tija na uzalishaji katika mazao ya kilimo na mifugo kwa kuwa suala ya kupambana na njaa ni kipaumbele cha kwanza.

Bibi Kaduma aliongeza kuwa moja kati ya mafaniko ya utekelezaji wa mradi wa EAAPP ni  kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya kilimo na kusisitiza kuwa Serikali itajitahidi kuwawezesha wakulima wanaozalisha mbegu bora kufanya biashara hiyo kwa uhakika,  wakiwemo wa ndani na nje ya nchi kwa kuwa Tanzania imeshakuwa mwanachama wa Shirika la Kimataifa la Hakimiliki za Wagunduzi wa Mbegu za Kilimo na Mimea mingine Duniani, (UPOV - International Union for the Protection of New Varieties of Plants).

Naye Mjumbe mwengine wa Benki ya Dunia, Dkt. Joseph Oryokot kutoka nchini Uganda alisema tayari nchi za Tanzania na Uganda zimeshawasilisha maombi ya kuiomba Benki hiyo kufadhiri mradi huo kwa awamu ya pili na kuongeza kuwa  suala la kilimo na uhakika wa chakula ni agenda ya muhimu kwao na kwamba bila shaka Taasisi yao italifanyia kazi ombi hilo.

Dkt. Oryokot alipongeza hatua ya Serikali ya Tanzania kuahidi kuwasaidia wakulima wake ili wauze mbegu zao nje ya mipaka na kusisitiza ni vyema nchi wanachama wakawa na sauti ya pamoja ya kuwasaidia wakulima kutengeneza mitandao ya masoko katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kwamba bila ya kufanya hivyo, wakulima wengi, wataendelea kukandamizwa na walanguzi ambao wapo kila mahali.