Skip to main content
Habari na Matukio

KATIBU MKUU AITAKA TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI KUKAMILISHA MIRADI YA UMWAGILIAJI KWA WAKATI

Katibu Mkuu  wa Wizara ya Kilimo  Gerald Kusaya amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika taasisi tatu kukagua utekelezaji wa majukumu yake.

Kusaya ametembelea Tume ya Taifa ya umwagiliaji (NIRC), Mfuko wa Taifa wa Pembejeo (AGITF) na wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA).

Katika ziara hiyo Katibu Mkuu Kusaya amesisitiza ulazima wa watumishi wa Taasisi hizo kufanya kazi kwa bidii, kufuata taratibu, kanuni na sheria za kazi katika utumishi wa umma.

Pia amewataka watumishi hao kujiendeleza kielimu kwa kusoma kozi fupi na ndefu ili kuongeza ujuzi katika kazi zao kulingana na fani mbalimbali walizonazo.

“Watumishi tubadilike na tufanye kazi kwa bidii na yeyote atakayekwamisha miradi yetu isiendelee nitamfukuza kazi” Alikaririwa Katibu Mkuu KUsaya

Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Kusaya amesema kuwa ni vyema kukawa na miradi michache ambayo Tume itaweza kuiendesha kuliko kuwa na miradi mingi isiyokuwa na tija.

Kusaya ameyasema hayo leo Tarehe 15 Aprili 2020 baada ya kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Ndg Nicodemus Kaal  kuwa Tume hiyo ina miradi 2678 ambayo ipo sehemu mbalimbali nchini ikiwemomkoani Kilimanjaro.

“Tuwe na miradi michache ambayo tutaimaliza, kwenye utendaji  wangu lazima miradi yote iishe, kati ya hiyo miradi 2678 utakuta labda miradi 10 ndio imekamilika” alisisitiza Kusaya

Aidha, amemtaka Mhasibu kumpatia ripoti ya mitambo yote  56 ambayo ipo na malori 37 na sababu ya mitambo hiyo kutokukamilika kwa wakati na gharama ambazo wanawalipa wakandarasi hao.

MWISHO