Skip to main content
Habari na Matukio

KATIBU MKUU KILIMO AKERWA TFRA KUWA NA IDADI KUBWA YA WATENDAJI WANAOKAIMU

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Kusaya ameonyesha waziwazi kukerwa na Watendaji wengi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) kukaimu kwenye nafasi zao na kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Kilimo kushirikiana na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania ili kushughulikia kero hiyo.

Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya amesema kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa Wizara ya Kilimo, amekutana na changamoto ya Watendaji wengi kukaimu katika nafasi zao na kuongeza kuwa; hafuraishwi kuona jambo hilo likiendelea na kusisitiza kuwa sasa ni muda muhafaka wa kumaliza changamoto hiyo.

“Baada ya kuapishwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli siku iliyofuata, nilikuja ofisini, Dodoma kwa ajili ya kuanza kazi rasmi nilishuhudia Watendaji wengi, wakijitambulisha kuwa Makaimu; kukaimu si jambo geni na ni sehemu ya mchakato wa kumpata Kiongozi bora lakini unakuta Mtendaji anakaimu zaidi ya miezi sita (6) na wengine mpaka miaka mitatu (3) hii si sawa.” Amesisitiza Katibu Mkuu.

“Napenda mfahamu kuwa, Sekta ya Kilimo inategemea nguvu kazi ya Watendaji wanaojiamini na wenye matumaini, sasa ukiwa na Mtendaji ambaye, anakaimu kwa muda mrefu ni vigumu kujituma na kuwa mbunifu kwa sababu hiyo inakuwa ngumu kuleta tija kwenye Taasisi nyeti kama Wizara yetu ya Kilimo”. Amesisitiza Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu Bwana Gerald Kusaya ameongeza kuwa haoni sababu kwa nini Mtendaji athibitishwi ili aongoze kama uwezo, sifa na vigezo anavyo na kuagiza kushughulikiwa mara moja kero hiyo.

“Mkurugenzi Mkuu wa TFRA, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Kilimo na wa TFRA jambo hili lipo ndani ya uwezo wenu, litatueni haraka na kama kuna mahali mtakwama, nipo na mnifahamishe haraka iwezekanavyo; binafsi sipendi kuongoza Watendaji wanaokamimu si Wizarani Makao Makuu lakini pia hadi kwenye Taasisi za Wizara kama TRFA.” Amemalizia Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bwana Gerald Musabila Kusaya yupo kwenye ziara ya kuzitembelea Taasisi za Wizara ya Kilimo kwa lengo la kujitambulisha na kuwafaham Watumishi wa Taasisi ambapo leo (Jana) alitembelea Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Kipawa, Bodi ya Chai pamoja na Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai (TSHTIDA). Taasisi zote hizi zipo Jijini, Dar es Salaam.

Kesho atazitembelea Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Mfuko wa Taifa wa Pemebejo za Kilimo (AGITF), Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Makao Makuu. Taasisi zote hizi zipo Jijini, Dodoma.