Skip to main content
Habari na Matukio

KATIBU MKUU WA KILIMO BW.KUSAYA ASAINI RANDAMA YA MASHIRIKIANO BAINA YA WIZARA YA KILIMO NA SIDO

Katika kuhakikisha tatizo la sumukuvu linapungua hapa nchini, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya  leo (18/06/2020) amesaini mkataba wa ujenzi wa vihenge baina ya Wizara ya Kilimo na  Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO) jijini Dodoma.

Katibu Kusaya amesema kuwa lengo la warsha hiyo ni kusaini mikataba miwili ambayo inahusiana na mradi wa Sumukuvu katika kuimarisha usalama wa chakula na kusaidia kutengeneza vihenge. Hata hivyo Kusaya amesema mradi wa sumukuvu umetokana na kutohifadhi  vizuri chakula hasa katika mazao ya karanga na mahindi.

Aidha, Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 3.8 ambazo zitapelekwa  SIDO ili ziweze kusaidia kutoa mafunzo ya vihenge. Mkurugenzi wa SIDO Mhandisi. Profesa. Sylvester Mpanduji amesema Kiwanda hicho kitashiriki katika kutoa teknolojia, mafunzo, mikopo na kuhamasisha kutafuta masoko ili viwanda vidogo vipate wanunuzi.

Pia Kusaya amesema atazifuatilia fedha hizo ili kuona zinatumika vizuri na kuwataka watendaji wakuu wa SIDO kutimiza wajibu wao katika suala hili. Na amewasisitizia wananchi juu ya upendo alionao Mhe. Rais Magufuli kwa kuwapatia mradi huu ambao utasaidia kutokomeza tatizo hili.

 “ Hizi fedha sio zetu ni fedha za umma, za walipa kodi” alisema Kusaya

Katibu Kusaya ametoa wito kwa wananchi kwamba miradi itakapokamilika waitunze ili iwasaidie kwani tatizo hili la sumukuvu ni kubwa. Aidha,katika kutekeleza mradi huu Kusaya amesema Wizara itashirikiana na taasisi nyingi kama SIDO, VETA, TPRI, TARI, CPB, TBS na taasisi nyingine ambazo zinahusiana na masuala ya chakula.

“ Ni jukumu letu sisi Wizara kuhakikisha hii mipango tunayopanga inakamilika kwa wakati na sisi Wizara ya Kilimo hatuwezi kutekeleza peke yetu ndio maana tunashirikiana na wananchi” alisema Kusaya

Wakati akihitimisha  Katibu Mkuu huyo amesema baada ya siku chache Wizara itasaini tena mkataba na wakandarasi ambao wataenda kujenga maabara na Kituo mahiri cha Usimamizi wa mazao ya nafaka.

Mratibu wa Mradi wa Sumukuvu  Bw. Clepin Josephat amesema VETA inatarajia kutoa mafunzo kwa vijana 400 ambapo watapata mafunzo ya teknolojia ya kutengeneza vihenge na itawasaidia katika kuwapatia ajira vijana hao