Skip to main content
Habari na Matukio

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Mhandisi Mtigumwe amtembelea Msindikaji wa Nafaka Wilayani Busega

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe hivi karibuni akiwa njiani kuelekea mkoani Simiyu amepata fursa ya kutembelea kiwanda cha Mwekezaji mzawa wa kusindika Nafaka Bwana Deogratius Kumalija katika Wilaya ya Busega.

 

Akiwa kiwandani hapo Mhandisi Mtigumwe alipata maelezo kutoka kwa mmiliki huyo kuwa ameamua kujikita katika usindikaji wa mazao ya Nafaka kutokana na fursa iliyopo katika kuongeza thamani ya mazao hayo hususan mahindi na mpunga.

 

Bwana Kumalija aliendelea kusema kuwa kiwanda hicho cha mpunga kina uwezo wa kukoboa Tani 28 kwa siku na alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kupanga madaraja ambapo kiwanda cha kusaga mahindi kipo katika ujenzi na punde kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kusaga tani zaidi ya 30 za mahindi kwa siku.

 

Alisema kuwa Viwanda Hivyo vitasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na kuondokana na nchi kuendelea kuuza mazao ghafi.

 

Kadhalika, Mhandisi Mtigumwe alimpongeza Mwekezaji huyo kuwa aendelee na uwekezaji huo pia Serikali imekuwa ikisisitiza kuyaongezea thamani mazao ya kilimo.

 

Hivyo mwekezaji kama Bw Kumalija anatimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwa na uchumi wa kati kupitia Sekta ya Viwanda ili viongeze ajira na kuhamasisha Wakulima kulima wakiwa na uhakika wa mazao yao kupata soko na kuyaongezea thamani.