Skip to main content
Habari na Matukio

KUANZIA TAREHE 15 AGOSTI, 2022 WAKULIMA WATANUNUA MBOLEA KWA NUSU BEI – WAZIRI BASHE

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe leo tarehe 9 Agosti, 2022 akiwa kwenye ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa katika Kijiji cha Iwawa Mabehewani wilayani Makete mkoani Njombe amewaambia Wakulima kuwa, kuanzia tarehe 15 Agosti, 2022 bei ya mbolea zote, itashuka kwa zaidi ya asilimia 50.

Kauli ya Waziri Bashe iliamsha ndelemo na vifijo kwa umati wa Wananchi walikuwa wakifuatilia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mama Samia Suluhu Hassan.

Waziri Bashe ametaja bei za mbolea hizo kuwa; Mbolea ya kupandia (DAP) ambayo awali ilikuwa ikiuzwa kati ya shilingi 131,676 hadi 140,000 sasa itauzwa kwa shilingi 70,000.

Bei ya mbolea ya kukuzia (UREA) ambayo awali ilikuwa, ikiuzwa kati ya shilingi 110,000 hadi 124,724 sasa itauzwa kwa shilingi 70,000.

Waziri Bashe ameongeza kuwa bei ya mbolea aina ya CAN ambayo awali ikuwa ikiuzwa kati ya shilingi 108,156 hadi 110,000 sasa itauzwa kwa shilingi 60,000.

Waziri Bashe amesema bei imeshuka kwa kiwango kikubwa inatokana na Serikali ya Awamu ya Sita kutenga fedha kiasi cha shilingi Bilioni 150 kwa ajili ya kumpunguzia makali Mkulima na kumpaa unafuu ili azalishe kwa wingi na kwa tija.

Waziri bashe ameongeza kuwa mbolea zote za kukuzia aina zote za YARA zilizokuwa zikiuzwa hadi shilingi 122,695 sasa zitauzwa shilingi 70,000 pamoja na mbolea za NPK huku mbolea aina SA iliyokuwa ikiuzwa shilingi 8282,852 sasa itauzwa shilingi 50,000.

Waziri Bashe ametoa onyo kwa Wafanyabiashara na Mawakala wote wa mbolea kuhakikisha wanajisajiri kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea (TFRA) na wale wa viuatilifu wanapaswa kujisajiri kwa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu (TPHPA) ili kutenda haki kwa Wakulima.

“Uonevu kwa Wakulima sasa basi; Niwaombe Wakuu wa mikoa, Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya pamoja na Wakuu wa wilaya tusaidiane kwenye jambo hili ili tuwasaidie Wakulima wetu”. 
“Serikali haitasita kuwafutia leseni, Wafanyabiashara wasiofuata utaratibu”. Amekaririwa Waziri Bashe.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu yupo mkoani Njombe kwa ziara ya siku tatu ambapo leo, amefungua rasmi Barabara ya Njombe, Moronga – Makete yenye urefu wa kilometa 107 katika Kijiji cha Iwawa Mabehewani na kusema kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisha usafiri kwa Wananchi, mazao ya kilimo na kuchangia kupungua makali ya bei kwa walaji.